Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akisalimiana na Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo wakati wa kikao kazi cha tathimini ya Utekelezaji wa shughuli za Vyuo hivyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini katika kikao kazi cha tathimini ya Utekelezaji wa shughuli za Vyuo hivyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mkoani Morogoro.
*************************
Na Mwandishi Wetu Morogoro
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini vimetakiwa kuwa chachu ya kubadilisha fikra katika jamii ili iweze kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao ili kujiletea maendeleo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu mkoani Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha tathimini ya Utekelezaji wa shughuli za Vyuo hivyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Dkt. Jingu amesema kuwa Vyuo hivyo vinafanya kazi nzuri ya kuzalisha wataalam mahiri wa Maendeleo ya Jamii, ambao wamekuwa chachu katika kuhamasisha na kuamsha ari ya wananchi kushirki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu.
“Serikali imewaamini na ina matarajio makubwa kutoka kwenu na majukumu mliyopewa ni makubwa na mnahitaji kuyatekeleza kwa uadilifu na weledi mkubwa” alisema Dkt. Jingu
Ameongeza kuwa Serikali inahimiza Wataalamu wanaozaliwa na Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaozalishwa nchini kwa ajili ya kutatua changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania.
“Ninasisitiza kuendelea kuimarisha vituo atamizi kwa ajili ya kukuza na kuendeleza wabunifu, ili kupitia ubunifu huo waweze kuanzisha kampuni zitakazowasaidia kujiajiri na kuajiri wengine” alisisitiza Dkt. Jingu
Aidha Dkt. Jingu ametolea mfano mmoja wa mradi wa ubunifu wa mashine inayotumia mfumo wa maji kusukuma maji tofauti na mashine nyingine zinazotumia nishati ya mafuta katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale, iliyosaidia kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo yanayozunguka Chuo hicho.
”Nimeambiwa kuwa Mashine hii ina uwezo wa kusafirisha maji kwa umbali wa kilometa moja na kujaza lita 1,200 kwa saa na ina uwezo wa kufanya kazi usiku na mchana hili ni jambo zuri kwani tunatatua changamoto ya upatikanaji wa maji” alisema Dkt. Jingu
Vilevile Dkt. Jingu ameeleza kuwa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vimetekeleza agizo la kuanzisha programu ya Uanagenzi ambayo pia imesisitizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025 ambapo hadi sasa takribani vijana wetu 40 wamepata ajira katika Taasisi na Kampuni mbalimbali kupitia mafunzo ya Uanagenzi.
“Natoa rai kuongeza jitihada za kuwaunganisha wanafunzi na wahitimu wengi zaidi kwenye Taasisi mbalimbali, ili wazidi kupata ujuzi utakaowawezesha kuajirika kirahisi zaidi, kujiajiri na kuajiri wengine” alisema Dkt. Jingu
Pia Dkt. Jingu amesisitiza kuwa Wizara inathamini mchango wa Taasisi na Vyuo wa kutatua changamoto katika jamii kupitia dhana ya Ushirikishaji Jamii kwa kupitia utekelezaji wa dhana hii imewawezesha wanawake na vijana kuunda vikundi mbalimbali vya kijasiriamali na kuwapa ujuzi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kutatua changamoto zinawazowakabili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii amesema kikao kazi hicho kinalenga katika kufanya tathimini ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kubaini maeneo ambayo yamefanywa vizuri na yale yenye changamoto na kitatumika kuwajengea uwezo Wakuu wa Vyuo wa namna ya kuboresha ili kuleta tija na ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu hayo.
Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Elibariki Ulomi ameishukuru Wizara kwa kuviwezesha Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kutoa mafunzo kwa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ili waweze kutatua changamoto zinazokabili jamii kutokana na programu tofauti zilizotolewa kwa Watalaam Vyuoni humo.