Mthamini kutoka ofisi ya kamishna wa ardhi mkoa wa Tabora Erick Michael Chambua wa kwanza kulia akikagua baadhi ya hati ya viwanja wa pili ni mkuu wa idara ya ardhi na maliasili halmashauri ya Igunga Jahulula Edward Jahulula aliyeshika maiki akiwa katika mtaa wa stoo
*****************************
Wananchi wa wilayani Igunga mkoani Tabora wameiomba serikali kushusha huduma ya kuandaliwa hati za viwanja kwenye wilaya yao ya Igunga kwani kwa sasa ina walazimu kufuata huduma hiyo Tabora mjini ambapo umbali wake ni kilomita mianne kwenda na kurudi hali inayochangia kushindwa kumudu gharama za nauli na malazi.
Maombi haya yametolwa na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaa wa stoo kata ya Igunga mjini wakati wa kugawa hati miliki za ardhi baada ya maeneo yao kurasimishwa rasmi ambapo Cheyo Pius, Zainabu Haruna walisema endapo huduma itasogezwa katika wilaya yao itasaidia wao kutembea umbali mrefu ambapo husababisha baadhi ya shughuli za uchumi kukwama kutokana na muda mwingi kwenda Tabora mjini kufuatilia hati zao.
Aidha Cheyo alibainisha kuwa hivi sasa wanaishukuru ofisi ya kamishna wa ardhi mkoa wa Tabora kuanza kuwafuata wananchi kwa kuwapelekea huduma hiyo katika maeneo yao ambapo amebainisha kuwa hali hiyo itasaidia kuongezeka mapato mengi ya serikali kutokana na malipo ya hati hizo.
Naye mkuu wa idara ya ardhi na maliasili halmashauri ya wilaya ya Igunga Jahulula Edward alisema benki ya NMB itawasaidia wananchi kulipia gharama za urasimishaji na umilikishaji na huku akitaja idadi ya viwanja vilivyorasimishwa kuwa ni elfu kumi na moja (11,000).
Sambamba na hayo Jahulula Edward aliwataka wananchi kuachana na baadhi ya madalali wa viwanja ambao wamekuwa wakileta migogoro katika Idara ya ardhi na kusema kuwa shida zote za ardhi zinatatuliwa na ofisi ya idara ya ardhi huku akitoa onyo kali kwa madalali wa viwanja kuacha mara moja tabia ya kuwatapeli baadhi ya wananchi.
Kwa upande wake mthamini kutoka ofisi ya kamishina wa ardhi mkoa wa Tabora Erick Michael C ambua alisema hivi sasa wameamua kusogeza huduma kwa kwenda kila wilaya kugawa hati za viwanja ili kuwarahisishia wananchi kutotembea umbali mrefu.
“Ndugu zangu wananchi kwanza napenda kuwashukuru kwa uvumilivu wenu, hivyo sisi kutoka ofisi ya kamishna tumepokea kilio chenu tumeamua kutembea kila wilaya kwa ajili ya kutoa huduma hiyo hivyo naomba muendelee kuiamini serikali kuwa hati zenu zote mtazipata”.
Hata hivyo katika mkutano huo mthamini kutoka ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora aligawa hati 38 za viwanja huku akiwataka wananchi wengine ambao hawajapata hati zao wafike ofisi ya halmashauri ya wilaya Igunga kwa ajili ya kuchukua hati zao.
Nae Diwani wa kata ya Igunga Athumani Mdoe CCM alisema serikali inayoongozwa na na Rais Samia Suluhu iko imara kwa kuhakikishia wananchi kuwa hakuna mwananchi yoyote atakosa hati na kuwataka kulipa kodi za viwanja pasipo usumbufu kwa vile fedha hizo zitarudi kufanya maendeleo