************************
Na Silvia Mchuruza,
Muleba,Kagera.
Wananchi wa kijiji cha Buhuma, kata ya Nyakatanga Wilaya ya Muleba wamehimizwa kujitolea kumalizia ujenzi wa zahanati ya kijiji ambayo imekaa muda mrefu bila kutumika ili iweze kuanza kutoa huduma na kuwaondolea changamoto ya kufuata huduma za afya umbali mrefu katika maeneo mengine.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la zahanati ya kijiji Buhume Mkuu wa wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila amewahimiza na kuwapa moyo wananchi wa kijiji hicho kujenga choo pamoja na kichomea taka katika eneo la zahanati ambayo ilijengwa kwa ushirikiano wa World Vision, Mchango wa Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini na Nguvu ya wananchi ambapo majengo yamekaa kwa muda mrefu bila kutumika.
“Mwenyekiti fanya kazi choo kijengwe, hamasisha wananchi kujitolea, nami nitawachangia mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya choo na kichomea taka. Mkikamilisha nawaletea muuguzi. Haiwezekani jengo likae miaka mitano bila kutumika kwa kukosa choo na kichomea taka wakati hakuna zahanati ndani ya kata nzima,” amesema Mhe. Nguvila.
Aidha, katika mkutano huo wafugaji wamelalamikiwa na wananchi kwa vitendo vyao vya kuingiza mifugo katika mashamba yao. Hivyo amemuagiza Afisa Kilimo kuacha namba ya simu kwa ajili ya mawasiliano ili mifugo ikiingia kwenye mashamba ya wananchi waweze kumpigia ili afike kwenye shamba na kufanya uthamini ili yule aliyeathiriwa na mifugo kula mazao yake alipwe fidia. Pia aliwasihi wafugaji waache mara moja tabia ya kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Ndg. Daudi Kingu amewashauri wataalamu ndani ya Kata hiyo, Afisa kilimo wa kijiji, Watendaji pamoja na Afisa Tarafa waanze kutoa elimu kwa wafugaji wenye ng’ombe wengi kuwaondoa ng’ombe katika eneo la kijiji na kuwapeleka kwenye ranchi za mifugo ili kuepusha migogoro baina yao na wakulima.
Naye Mhe. Nguvila amewaeleza wafugaji wenye ng’ombe wengi kuanzia 500 kwenye eneo la kijiji kuunda vikundi vya ushirika na wafugaji wengine ili waweze kupeleka mifugo yao kwenye vitalu vya mifugo na hasa kwenye eneo la ranchi ya Mifugo la Mwisa II.
Afisa Lishe wa wilaya Ndg. Tigelelwa Robinson amewahimiza wananchi wa kijiji hicho kutekeleza mpango wa kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni ili kuwawezesha kusoma vizuri na hata kuwa na afya bora. Aidha, amewahimiza wazazi kuhakikisha wanachanga vyakula ili huduma ya chakula iweze kutolewa kwa wanafunzi wanapokuwa shule.
Afisa Maendeleo ya Jamii Ndg. Frank Masebo ametoa elimu kwa wananchi juu ya mambo ya kuzingatia kwa ajili ya kupata mikopo isiyo na riba ya akina Mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu kuwa wanatakiwa kuwa na vikundi yenye watu kuanzia watano hadi ishirini na tano, kuwa na biashara, kufungua akaunti ya benki na kuwa na katiba ya kikundi ili kuweza kupatiwa mikopo inayotolewa na Halmashauri bila riba na kuanza kurejesha baada ya miezi mitatu.