……………………………………………………………
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wadau wengine limefanikiwa kudhibiti mauaji ya albino na vikongwe baada ya kuanza kutoa elimu sahihi kwa waganga wa tiba asili kuhusu madhara ya ramli chonganishi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi George Kyando amesema baada ya kubaini kuwa vifo vya albino na vikongwe vinachangiwa na ramli chonganishi, Jeshi hilo kwa kushirikiana na wadau wengine lilijikita kwenye utoaji wa elimu sahihi kwa waganga wa tiba asili.
Amesema ramli chonganishi ilikuwa inachochea chuki miongoni mwa wananchi hivyo kusababisha mauaji kwa vikongwe kutokana na visasi na imani potofu .
“Tulifanya sensa na tukawashauri waunde uongozi ili waganga wote wajisajili na tukigundua kunamauaji yametokewa ni imani za kishirikina waganga wote wa eneo hilo wanapatashida sisi kitengo cha Polisi jamii kinapita kutoa elimu kwamba waganga wote wajiepushe na imani za kishirikina mtu akija kwako wewe mpe dawa, mtibu tu kumwambia aliyefanya hivi ni fulani huo ni uchonganishi”.
Kamanda Kyando ameonya waganga watakaobainika kukiuka maelekezo ya serikali watafungiwa vibali vyao na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi hatuna ugomvi na hatupingi tiba asili lakini epukeni kutoa ramli chonganishi shughulikeni na ugonjwa na mganga yeyote tutakea mbaini mkoa huu ambaye anajihusisha na hizo ramli tutamuondoa kwenye hiyo biashara akafanye kazi nyingine”.