…………………………………………………………..
Na Silvia Mchuruza,Bukoba.
Wananchi wa kijiji cha Ilemela kata ya Gwanseli wilaya ya Muleba wamehimizwa kuachana na tabia ya kuvamia ardhi bila kufuata sheria huku akiwataka viongozi wa Serikali ya kijiji kuacha mara moja kugawa ardhi ya kijiji, hali inayosababisha migogoro ya ardhi na kutoelewana baina ya viongozi na wananchi wanaowaongoza.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa ofisi ya kijiji cha Ilemela kwa lengo la kutatua kero za wananchi ambao wamekuwa wakilalamikia uongozi wa kijiji hicho kugawa ardhi pasipo kufuata utaratibu.
Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Nguvila amewambia wananchi hao kuwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi mwananchi hatakiwi kumiliki zaidi ya eneo la ekari 50, Serikali ya kijiji kupitia vikao na mkutano mkuu wa kijiji wana mamlaka ya kumpa mtu aliyeomba ardhi ekari chini ya 50. Mamlaka ya kijiji inaweza kutoa ardhi na ardhi hiyo itolewe kwa ridhaa ya mkutano mkuu. Kama kuna watu wamejimilikisha ardhi bila kufuata huo utaratibu watanyang’anywa maeneo hayo na kuyarudisha kuwa chini ya himaya ya Serikali ya Kijiji.
“Katika kero zilizotolewa na wananchi wametajwa watu wengi waliojichukulia maeneo bila kufuata utaratibu. Sasa naunda kamati ya uchunguzi ili ije hapa kufanya uchunguzi kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 08.11.2021 na kamati hiyo itakuwa na mtu wa TAKUKURU kwa sababu kutokana na maelezo mengi yaliyotolewa na wananchi inaonesha kabisa rushwa inanukia hapa. Pia kamati itakuwa na mtaalam wa Ardhi ambaye ataongoza, atasanifu na kuhakiki taratibu zote kama zilifuatwa za utoaji wa ardhi.
Ndani ya kamati kutakuwa na mjumbe kutoka jeshi la Polisi, Afisa wa Usalama, Afisa Utumishi, Afisa Tarafa, Mtendaji wa Kata pamoja na Mhe. Diwani kwa ajili ya kutoa ushirikiano.
Baada ya uchunguzi kamati hiyo itasoma taarifa ya uchunguzi kwenye mkutano wa hadhara kama huu” ameeleza Mhe. Nguvila.
Sambamba na hayo amewahimiza wananchi wa kijiji hicho kuchangamkia fursa ya kilimo hasa kwa kupanda mibuni pamoja na kilimo cha parachichi ili iwainue kiuchumi.
Pia amemuagiza Mtendaji wa kijiji hicho kuhakikisha anaandaa taarifa ya mapato na matumizi na kuitisha mkutano wa hadhara wa kijiji ili wananchi waweze kusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji chao.
Naye, Afisa Ustawi wa Jamii Ndg. Frank Masebo ametoa elimu juu ya suala la mikopo isiyo na riba kwa akina mama vijana na watu wenye ulemavu na kuwasihi makundi hayo kuunda vikundi kwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti ya benki, kuwa na katiba ya kikundi na kisha kusajili kikundi ambapo amewahimiza pia kutotumia vibaya mikopo hiyo.
Mkuu wa TAKUKURU wilayani Muleba Bw. Said Lipunjaje amewahimiza viongozi kutokuwa na tamaa ya kutaka kujinufaisha na uongozi huku akiwasihi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ambapo amewambia kuwa matumizi mabaya ya madaraka kosa katika makosa ya rushwa kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mwisho Mhe. Diwani wa Kata ya Gwanseli amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea ufafanuzi ikiwemo kuunda kamati ya kuchunguza kero za ardhi.