Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dotto James,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 6,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu kongamano la 25 la Utafiti na Biashara kuhusu ushindani wa Viwanda na Biashara litakalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu, Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Novemba 10,mwaka huu na kufunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango
Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk Donald Mmari,akifafanua jambo kuhusu kongamano la 25 la Utafiti na Biashara kuhusu ushindani wa Viwanda na Biashara litakalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu, Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Novemba 10,mwaka huu.
……………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Washiriki 200 kuhudhuria Kongamano la 25 la Utafiti na Biashara kuhusu ushindani wa Viwanda na Biashara linalotarajia kufanyika Novemba 10, mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dotto James,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu, Julius Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Amesema kuwa la kongamano hilo ni kuchochea na kukuza mijadala ya kisera na utafiti kuhusu viwanda na biashara kama sekta muhimu ya kuharakisha ukuaji uchumi na kichocheo cha mabadiliko ya kimuundo litahudhuriwa na washiriki 200.
”Kati ya washiriki 200 walioalikwa watakuwepo viongozi wakuu kutoka Serikali ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu ya vikwazo vya usafiri, waalikwa kutoka nje watashiriki kwa njia ya mtandao”amesema
Amesema kuwa kongamano hilo limebeba kaulimbiu isemayo Mapinduzi ya Uchumi wa Tanzania kupitia ushindani wa viwanda na biashara ambayo ni muhimu kwani inafungamana vyema na msukumo wa mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano unaosisitiza kuendeleza juhudi za kuleta mageuzi ya uchumi, kuboresha ushindani wa kitaifa kwa maendeleo ya watu.
“Viwanda na biashara shindani ndio vichocheo muhimu vya mabadiliko ya kimuundo na ukuaji. Hii inaelezea ushirikiano unaoendelea kati ya wizara ya viwanda na biashara na REPOA kwa warsha hii na programu nyingine za utafiti na kujenga uwezo juu sekta hizi,”alisema.
Amesema kuwa kongamano hizo zinaandaliwa na REPOA na kufanyika kila mwaka huwakutanisha watafiti wabobezi, watunga sera, washiriki wa maendeleo, AZAKI, Sekta binafsi na wasomi kutoka taasisi za elimu ya juu nchini na nje ya nchi ili kujadili masuala ya maendeleo, matokeo ya tafiti kutoka kwa watafiti waliobobea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk Donald Mmari amesema makongamano yaliyofanyika siku za nyuma yameleta mchango mkubwa kwa taifa na sekta ya viwanda na biashara kwa ujumla.