**************************
NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
BARAZA la madiwani katika Halmashauri ya mji Kibaha limemuomba Rais Mama Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala la baadhi ya watumishi wa tamisemi ambao wanafanya kazi kwa maslahi yao binafsi na kupelekea kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha Mussa Ndomba alisema kwamba kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya miradi katika sekta ya elimu kukwama kutokana na kuwepo kwa hali hiyo.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao Cha baraza la madiwani ambacho kilihudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali.wakuu wa idara madiwani kutoka kata zote 14 pamoja na viongozi wengine wa chama.
Ndomba akiezea zaidi kuhusiana na athari ambazo zimekuwa zikiwakabili alifafanua kuwa fedha ambazo zinakuwa zinatengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wanashanga zinapelekwa katika maeneo mengine ambayo awajayapa vipaumbele.
“tunamuomba kwa dhati Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan aweze kutusaidia kwani kuna baadhi ya watumishi wa tamisemi wana athiri na kukwamisha sana miradi yetu ya maendeleo kwa maslahi yao binafsi tunaomba bajeti zetu za fedha tunazotengewa ziheshimiwe na zilizotumika kinyume zirejeshwe,”alisema Ndomba.
Pia alisema kuwa wanashangaa fedha ambazo wanaziomba kutoka serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo zinachepushwa bila sababu na kwenda katika maeneo mengine tofauti kabisa na jinsi walivyoomba kwa matumizi yao.
“Tumeweza kubaini kwamba Kuna mtumishi mmoja kutoka tamisemi amekuwa anatuathiri Sana katika kutekeleza miradi yetu ya maendeleo maana tunaomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Madara lakini zikiletwa zinachepushwa na kwenda katika maeneo mengine kwa hivyo tunamuomba Rais wetu atusaidie,”alisema Ndomba.
Alibainishwa kuwa kwa Mara ya kwanza walitapatwa na changamoto kwa kuathirika baada ya kupata kiasi Cha shilingi milioni 561 lakini fedha hizo zilikwenda katika maeneo mengine hivyo kupelekea miradi ya shule za kata kuweza kukwama.
Aidha alisema kwamba anashangaa Kuna fedha za Uviko 19 ambazo zilitolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa madara zimetumika tofauti kabisa na maombi ya bajeti yao hivyo Jambo linatakiwa kufanyiwa kazi.
“Kikubwa hapa hili Jambo kwa upande wetu linatuathiri Sana katika utekelezaji wa majukumu yetu ya miradi ya maendeleo tunachomuomba Rais wetu mpendwa atusaidie katika hili maana atuwezi kupanga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule fulani alafu fedha ikija inachepushwa kwingine,”alibainisha Ndomba.
Nao baadhi ya madiwani wa halmashauri ya mji Kibaha wameunga mkono na kuazimia kwa pamoja fedha zote ambazo wanazipanga katika bajeti zao ziweze kutumika Kama zilivyopangwa na sio vinginevyo.