**************************
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amezindua Kituo cha Usambasaji wa mbegu za kilimo Mkoa wa Shinyanga pamoja na kupokea Shehena ya zaidi ya tani 100 (kilo 190,000) ya mbegu bora za Mahindi na Alizeti kutoka Wakala wa Mbegu za Kilimo (Agricultural Seed Agency – ASA).
Uzinduzi huo umefanyika Ijumaa Oktoba 29,2021 katika Ghala la Chakula (NFRA) Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa kilimo mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mjema amesema Kituo cha Usambazaji wa mbegu za kilimo itawezesha upatikanaji wa mbegu bora kwa bei nafuu huku akiwataka Maafisa Kilimo kutokaa ofisini bali waende kwa wakulima ili mbegu hizo zitumike vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Mbegu hizi bora za kilimo zimekuja katika wakati muafaka kwani msimu wa kilimo umeanza. Shinyanga kuna ukame hivyo ni lazima tulime kimkakati. Tunamshukuru Mhe. Rais Samia katurahisishia kwa kutuletea mbegu hizi za kimkakati ambazo ni za muda mfupi tu alizeti miezi mine na mahindi miezi mitatu tu unavuna”,amesema.
“Tunashukuru kupata mbegu hizi bora, twendeni tukalime ili tuwe na chakula. Tunataka tulime ili tusiwe na njaa, haitakubalika hapa Shinyanga tuonekane hatuna chakula wakati mbegu bora tumeletewa. Shinyanga tunataka mtetemo wa maendeleo (Vibe)”,ameongeza Mhe. Mjema.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga ametumia fursa hiyo kuishukuru ASA kwa kuleta shehena ya mbegu bora za kilimo na kuiomba kuendelea kuleta mbegu za mazao yanayostahimili ukame huku akiwasihi wananchi kutumia mbegu hizo ili kuondokana na umaskini.
“Mbegu bora za kilimo zitakuwa zinauzwa kwenye maghala ya chakula na tutahakikisha wakulima waliopo pembezoni wanapata mbegu hizi ili waweze kulima kwa tija na kuondokana na umaskini”,amesema Mjema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dkt. Sophia Kashenge amesema kwa kuona umuhimu wa matumizi ya mbegu bora katika eneo la Kanda ya Ziwa umeona ni vyema kuwa na eneo maalumu litakalotumika kusambaza mbegu hivyo kwa kuanzia wamezindua Kituo cha Shinyanga ili kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora kwa bei nafuu kwa eneo hilo la Kanda ya Ziwa.
“Kwa awamu ya kwanza tumeleta shehena ya kilo 190,000 za mbegu za kilimo ambapo ni kwa mara ya Kwanza kwetu kusafirisha kwa kutumia Treni. Kati ya hizo kilo 20,000 ni mbegu bora za Alizeti (Standard seeds) ambazo zimeongezwa uwezo wa mkubwa wa kustahili visumbufu mbalimbali na kilo moja ya alizeti itauzwa shilingi 3500. Lakini kilo 89,000 ni za Mbegu bora ya mahindi (Situka M1) ambayo yanayostahimili ukame ambapo kilo moja ya mbegu hizi za mahindi itauzwa shilingi 2700”,ameeleza Dkt. Kashenge.
“ASA ina vituo mbalimbali vya usambazaji wa mbegu bora zinazozalishwa katika mashamba yake. Miongoni mwa vituo hivi vya usambazaji ni pamoja na vituo vyote vya uzalishaji katika mikoa mbalimbali na sasa kituo hiki cha Shinyanga kitakuwa msaada kwa maeneo ya Kanda ya Ziwa”,amesema Dkt. Kashenge.
Dkt. Kashenge ametumia fursa hiyo kuwashauri wakulima kutumia mbinu bora za kilimo ili mbegu hizo ziweze kuleta tija huku
Amesema ASA ambayo makao makuu yake yapo Mkoani Morogoro, kupitia mashamba yake 18 huzalisha mbegu za mazao zaidi ya 40 yakiwemo mahindi, mpunga,alizeti, soya, michikichi, maharage,mbogamboga,ufuta, karanga,mtama, kunde,choroko,mbaazi na mbegu za pamba kulingana na uwezo na mahitaji kwa wakati husika.
Aidha amesema ASA inahitaji eneo la Hekta 200,000 ili iendelee kuzalisha mbegu za kilimo nyingi zaidi ili kuhakikisha kuwa kila mkulima analima kilimo chenye tija akitumia mbegu bora.
Akifafanua zaidi Dkt. Kashenge ameeleza kuwa Tasnia ya mbegu nchini Tanzania inaundwa na sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha mbegu bora zinapatikana katika ngazi zote kwa wakati ambapo sekta ya umma inajumuisha Taasisi za TARI yenye jukumu la kuzalisha mbegu mama, TOSCI yenye jukumu la kudhibiti ubora wa mbegu na ASA yenye jukumu la kuzalisha na kusambaza mbegu bora.
Hata hivyo amesema changamoto ya matumizi bora ya mbegu bora kwa wakulima imetokana na uelewa mdogo wa matumizi ya mbegu bora pamoja na uwezo mdogo wa wakulima kununua mbegu bora hivyo kufanya matumizi ya mbegu bora nchini kuwa chini.
“Licha ya kwamba matumizi ya mbegu bora bado ni changamoto kwa wakulima wengi kutokana na upatikanaji mdogo wa mbegu bora, ongezeko kubwa la uhamasishaji wa matumizi ya mbegu bora za kilimo umesababisha hamasa kubwa kwa wakulima kuhitaji mbegu bora za kilimo. Hali hii imesababisha uhitaji mkubwa wa mbegu za mazao mbalimbali ikiwemo mbegu za mafuta”,amesema Dkt. Kashenge.
Nao Wakuu wa wilaya Jasinta Mboneko (Shinyanga) na Joseph Mkude (Kishapu) wameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongoza na Rais Samia Suluhu kwa kuwapatia mbegu bora za kilimo huku wakiahidi kuwa watapeleka mbegu hizo kwa wakulima maeneo ya vijijini kwa bei ile ile ya shilingi 3500 kwa kilo moja ya mbegu za alizeti na shilingi 2700 kwa mbegu za mahindi.