………………………………………………………..
Na Mwandishii wetu, Hanang’
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, limemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za miradi ya maendeleo shilingi bilioni 3.5.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Rose Kamili akisoma tamko la shukrani kwenye kikao cha baraza la madiwani amesema fedha hizo zimetolewa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Kamili amesema shilingi bilioni 1.8 zitatumika kwenye ujenzi wa vyumba 68 za shule 28 za sekondari zenye upungufu wa madarasa na vyumba 24 katika shule tisa shikizi za msingi.
Amesema shilingi milioni 810 milioni zitatumika kwa ujenzi wa jingo la huduma za dharura, ununuzi wa mashine ya mionzi na ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa hospitali ya wilaya hiyo (Tumaini).
Amesema sh250 milioni zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha afya kwenye kata ya Gisambalang ambayo ipo pembezoni imepakana na wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
“Pia shilingi milioni 603 zitatumika kwa ujenzi wa miundombinu ya maji na vyoo katika vituo nane vya kutolea huduma za afya na ujenzi wa miundombinu wa shule mbili za sekondari,” amesema Kamili.
Amesema pia kwenye fedha hizo shilingi milioni 603 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kunawa mikono kwenye shule nane za msingi na uhamasishaji wa jamii kujikinga na Uviko-19.
Mbunge wa jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha hizo ambazo zitachochea maendeleo.
Mhandisi Hhayuma amesema kwa kupitia fedha hizo shilingi bilioni 3.5 zitatumika kwenye miradi hiyo ya maendeleo kwa namna moja au nyingine katika idara za elimu, afya na maji.
Diwani wa Tarafa ya Katesh July Songay amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwapatia fedha hizo ambazo baadhi zitatumika kuboresha shule shikizi za eneo hilo.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Hanang’ Mathew Darema amesema pamoja na kumshukuru Rais Samia, fedha hizo zitumike ipasavyo ili serikali iweze kuwaletea fedha nyingine.