…………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea kiasi cha sh bil 1.84 katika mgao wa fedha za UVIKO 19 kwa ajili ya kumaliza changamoto za sekta ya elimu.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana diwani wa kata ya Mbutu ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Lucas Bugota alisema kuwa Rais Samia ana dhamira ya dhati kumaliza kero zinazoikabili jamii katika sekta zote.
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kujenga jumla ya vyumba 92 vya madarasa vilivyokuwa vikihitajika na kutengeneza madawati 4600 ya kukalia watoto wote watakaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza.
Alifafanua kuwa mahitaji halisi ya halmashauri ili kuwezesha watoto wote watakaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kupata nafasi ilikuwa madarasa 92 kwa wilaya nzima kwa ajili ya shule zote 33 za sekondari za kata.
Aliongeza kuwa pia walikuwa na uhitaji wa jumla ya madawati 4600 yatakayotumiwa na wanafunzi hao, na halmashauri haikuwa na bajeti ya kutosheleza kununua madawati hayo kwa mkupuo mmoja.
‘Tunamshukuru sana mama yetu, Rais Samia kwa kutuletea kiasi hicho, hatukutegemea, tulikuwa tunahangaika usiku na mchana ili kuhakikisha watoto wote wanapata nafasi katika shule watakazopangiwa na si vinginevyo’, alisema.
Bugota alimpongeza Rais kwa kuwasaidia kumaliza kero hiyo kwani hapatakuwa na mwanafunzi hata mmoja atakayekosa nafasi, aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao katika shule watakazopangiwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Manonga Seif Gulamali alimpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia kiasi cha sh mil 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ziba kilichoko katika jimbo hilo ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
‘Mama yetu anafanya kazi kubwa sana, tutaendelea kumuunga mkono kwa yale yote anayoyafanya kwa manufaa ya wananchi wetu, ameahidi kumaliza kero za wananchi katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu na sasa anatekeleza’, alisema.
Alibainisha kuwa katika kuunga mkono juhudi hizo halmashauri ya wilaya hiyo inatararajia kuanza kujenga kituo cha afya Nanga kwa kutumia fedha zake za ndani ambapo wametenga jumla ya sh mil 400.