***************************
Na Eleuteri Mangi, Morogoro
Mashindano ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2021 kwa mbio za baiskeli imepata mabingwa wa mchezo huo ambapo kwa upande wa wanaume Omari Ligoneko kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ameibuka kidedea huku kwa upande wa wanawake bingwa ni Scolastica Hamis kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi).
Mbio hizo zimefanyika leo Oktoba 30, 2021 ambapo kwa upande wa wanaume ambao wameendesha baiskeli kwa umbali wa Kilometa 35 kuanzia kijiji cha Melela-Kololo wilayani Kilosa zimehitimishwa eneo la Mafiga Manispaa ya Morogoro wakati wanawake wameendesha baiskeli kwa umbali wa Kilometa 24.5 kuanzia Njiapanda ya Kilosa hadi eneo la Mafiga Manispaa ya Morogoro.
Bingwa huyo Omari Ligoneko wa mbio za baisketi wanaume anatoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi aliendesha baisketi kwa saa 1:10:08 huku mshindi wa pili akiwa ni Ezekiel Muhina kutoka Ofisi ya RAS Tanga ambaye alitumia saa 1:10:44 na mshindi wa tatu ni Siraji Mohamed kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye alitumia saa 1:12:23 kumaliza mbio hizo ambapo washiriki walikuwa 21.
Kwa upande wa wanawake bingwa kwa mbio hizo za Kilometa 24.4 ni Scolastica Hamis kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) ambaye alitumia saa 1:08:40, mshindi wa pili ni Betha Wilson kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) ambaye alitumia saa 1:09:10 na mshindi wa tatu ni Agness Mtulanye kutoka Wizara ya Nishati ambaye alitumia saa 1:10:00. ambapo washiriki walikuwa tisa.
Mbio hizo zimekuwa kivutio kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro kuanzia wilaya ya Kilosa hadi Manispaa ya Morogoro na viunga vyake ambao wanaendelea kupata burudani ya michezo ya SHIMIWI inayoendelea katika viwanja tofauti tofauti mjini hapo.
Katika mchezo wa bao kwa upande wa wanaume bingwa ni Emmanuel Komba kutoka Ofisi ya RAS Ruvuma ambaye alimshinda mpinzani wake Imani Mwaipaja mbaye ni mshindi wa pili katika mchezo huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Shamuni kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji).
Kwa upande wa wanawake katika mchezo wa bao bingwa ni Zamira Fundi kutoka Wizara ya Kilimo, mshindi wa pili ni May Naumbwa kutoka Ofisi ya RAS mkoa wa Lindi na mshindi wa tatu ni Asteria Mwang’ombe kutoka Ofisi ya RAS Morogoro.
Nusu fainali za mchezo wa mira wa miguu pamoja na netiboli zinatarajiwa kufanyika Oktoba 31 ambapo timu nne kila mchezo zimefika hatua hiyo ambazo ni Wizara ya Nishati, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati katika mchezo wa netiboli timu za Ofisi ya Rais Ikulu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hazina pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi zimefika hatua hiyo.
Mashindano ya SHIMIWI yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za SHIMIWI ambapo klabu zote zinazoshiriki mashindano hayo zimesajiliwa zimesajiliwa kwa Msajili wa Vyama vya Michezo chini ya kifungu 28 cha kanuni za usajili wa vyama vya michezo ya 1999 namba 3(b) ambacho kinasema Chama cha mchezo wowote hakitaruhusiwa kuendesha shughuli za michezo bila kusajiliwa.