Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Mashindano ya kuogelea ya Kanda ya Nne Afrika (Cana Africa Zone 4) yameanza kwa kushindo jijini Dare s Salaam huku waogeleaji wa Tanzania wakionyesha makali yao.
Mashindano hayo yanafanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Masaki yanashirikisha waogeleaji wa Tanzania zaidi ya 70.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya kuogelea, Alexander Mwaipasi alisema kuwa mashindano hayo yanashirikisha nchi zaidi ya 20 na amevutiwa na maendeleo ya waogeleaji wa Tanzania mpaka sasa.
Mwaipasi alisema kuwa waogeleaji wa Tanzania wameonyesha uwezo mkubwa na wanatarajia kupata matokeo mazuri mara baada ya kumalizika kwake.
Alisema kuwa wachezaji wengi wa Tanzania wameweza kupunguza muda wao wa kuogelea (PBs) na kuleta matumaini makubwa ya kukusanya pointi nyingi.
“Mpaka sasa nimevutiwa na ushindani wa waoegeaji wa Tanzania pamoja na ukweli kuwa wanashindana na waogeleaji wa nchi nyingine zaidi ya 20. Tutarajie matokeo mazuri na tunaamini kuwa tutafanya vizuri,” alisema Mwaipasi.
alisema kuwa wanashindana na nchi mbalimbali ambazo ni Afrika Kusini, Zambia, Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan na Uganda.
Pia kuna nchi kama Angola, Botswana, Comoros, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Seychelles, Eswatini na Zimbabwe.
Kwa mara ya kwanza, mashindano hayo yanaonyeshwa live kupitia Champion Rise televisheni kupitia link; https://www.youtube.com/watch?v=KXWrnXVNQE4 na hakuna mashabiki kutokana na zuio la ugonjwa wa Uviko 19.