Mke wa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo akizungumza katika Ufungaji wa Mafunzo ya Upambaji huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mke wa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo akimkabidhi Cheti cha Kuhitimu Mfunzo ya Upambaji Mwanafunzi Zubeda, katika hafla ya Ufungaji wa Mafunzo ya hayo, huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi kutoka Taasisi ya maswala ya Upambaji (Emmy Enrich Art ) Amina Amran Juma, akielezea lengo kuu la kutoa mafunzo ya Upambaji, wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mhitimu wa mafunzo ya Upambaji Habiba Foum Ali akisoma risala katika hafla ya Ufungaji wa Mafunzo ya Upambaji, huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waalikwa na Wahitimu wa Mafunzo ya Upambaji, waliyohudhuria hafla ya Ufungaji wa Mafunzo ya Upambaji katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
***************************
Na Mwashungi Tahir Maelezo 30-10-2021.
Mke wa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo amewataka akinamama kushiriki katika kazi za mikono kwa lengo la kujipatia riziki na kuepuka kuwa na ugumu Wa maisha.
Hayo ameyasema huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar wakati akifunga mafunzo ya upambaji kwa akinamama waliopata mafunzo hayo na kuwataka kuyatumia ili waweze kujikimu kimaisha na kiuchumi.
Amesema mwanamke ndio mlezi au kiongozi wa familiya hivyo asikae na kubweteka kusubiri baba ni lazima aitumie fursa zilizopo kwa kujipatia kujikimu kimaisha na kujikomboa kiuchumi yeye pamoja na familiya yake.kwa kujituma .
Hivyo amesema fursa waliyoipata wataweza kufaidika na Taifa litasimama na kuondosha udhalilishaji kwa kujiajiri kwa kutumia mafunzo hayo waliyojipatia ambayo ni ajira tosha na kuacha kusubiri ajira kutoka Serikalini.
Aidha amesema mama ni mtu mwenye kuheshimiwa kwani yeye ndio mshughulikiaji mkuu wa familiya na kuhakikisha watoto wake wanakuwa katika hali ya usalama kwa kuwafunza maadili yaliyo bora kuwaepusha kuiga mambo yasiyokuwa na maadili.
“Hakuna mama anayetaka watoto wake waingie katika vitendo visivyofaa hivyo mama kama mama atasimama kidete kuilinda familiya yake” alisema Mama Zainab Kombo .
Akitoa wito kwa vijana hao amewataka kuendeleza taaluma waliyoipata na kuhakikisha wanaifanyia kazi kwa moyo mmoja.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Emmy Enrich Art masuala ya upambaji Amina Amrani Juma amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwakusanya wanawake wenye mahitaji maalum, wajane na vijana ili waweze kujikimu kimaisha wao na familia zao.
Hivyo amewaasa vijana wasikate tamaa wapambane katika kujikomboa kimaisha kwa kutumia taaluma wanazopatiwa kwani Serikali haitoweza kuwaajiri wote.
Kwa upande wake msomaji wa risala Mwanafunzi Habiba Foum Ali amesema mafunzo hayo yamewashirikisha akinamama kutoka wilaya tatu ikiwemo Magharibi A na B pamoja na Mjini kwa lengo la kubadilisha maisha yao .
Akitoa changamoto amesema wana uhaba wa sehemu ya kufanyia mafunzo , na kukosa mashirikiano kwa baadhi ya viongozi kwani bado jumuiya hiyo ni changa wasaidiwe.
Na kwa upande wa mafanikio amesema wameweza kufaidika na taaluma hiyo ya upambaji na kuwataka wanawake wenzao kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hizo na kuweza kupata ujuzi.
Jumla ya wanafunzi 55 wamefanikiwa kuhitimu mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti.