Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi akizungumza wakati wa Mkutano wa Tano wa Jukwaa la Mawaziri wanaohusika na sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Oktoba 29, 2021.
Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobasi Katambi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Jukwaa la Mawaziri wanaohusika na sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Willington Chibebe akieleza jambo wakati wa mkutano huo.
Mawaziri wanaohusika na Sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashiriki (EAC) wakionesha Ripoti ya kikao cha jukwaa la Tano (5) la sekta hiyo lililofanyika Jijini Dar es Salaam, Oktoba 29, 2021. Wa tatu kutuka kushoto ni Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Uchumi na Uwekezaji) kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mudrik Soranga.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
*************************************
Na: Mwandishi Wetu: DAR ES SALAAM
Mkutano wa Tano wa Jukwaa la Mawaziri wa Sekta ya Kazi na Ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika Oktoba 30, 2021 jijini Dar es Salaam huku Mawaziri wakikubaliana kuendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na mikutano ya Wataalamu na Makatibu Wakuu ili lenga kupitia na kujadili utekelezaji wa miradi na programu katika sekta ya kazi na ajira pamoja na utekelezaji wa maagizo na maamuzi mbalimbali ya jukwaa hilo la Mawaziri linalohusika na kazi na ajira.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni muendelezo wa usimamizi wa sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yam waka 1999 katika utengamano wa jumuiya hiyo.
“Utekelezaji wa maagizo, mapendekezo na maamuzi mbalimbali yaliyotolewa yatasaidia kuboresha maeneo mbalimbali katika sekta hii ili kuleta mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ustawi ya jamii kwa nchi wanachama,” alisema Katambi
Aidha, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa katika vikao vilivyotangua vya Makatibu Wakuu na Wataalam kwa majadiliano mazuri ya utekelezaji wa mapendekezo, maagizo na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na kuamuliwa katika mikutano ya ngazi mbalimbali na vyombo vya kisera vya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sambamba na hayo Naibu Waziri Katambi alitumia fursa hiyo kuelezea namna Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyojizatiti katika kukuza sekta ya kazi na ajira kupitia miradi na programu mbalimbali zinazoanzishwa nchini.
Kikao hicho kimejadili na kukubaliana masuala yafuatayo ikiwemo Kuimarisha sera ya kuratibu masuala ya uhamaji nguvukazi ambayo itatoa fursa kwa vijana katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kujiajiri na kuajiriwa; Kuimarisha program ya kubadilishana wafanyakazi vijana ndani ya nchi wanachama; Kuimarisha na kuainisha Sheria za kazi ndani ya Jumuiya ili kulinda haki za wafanyakazi wageni ndani ya jumuiya hiyo na Kukamilisha mchakato wa kuratibu masuala ya uhamishaji wa mafao ya hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wanaohamia au kurudi nchini mwao.
Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi na wawakilishi kutoka nchi zote wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia Wataalamu na Wadau wa Utatu wa sekta ya kazi na ajira walishiriki, ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa Mawaziri uliongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobasi Katambi, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Uchumi na Uwekezaji) kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mudrik Soranga, Katibu Mkuu kutoka ofisi hiyo Tixon Nzunda pamoja na Wakuu wa Idara zinazojishughulisha na sekta hiyo.