Na Bashiri Salum, Singida
VITUO vya afya 15 na Hospitali tatu (3) vimejengwa mkoani Singida ili kutoa huduma ya dharura kwa wazazi na watoto ikiwa ni mkakati madhubuti wa kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya ya kutolea huduma ya afya ya mama na mtoto kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba, kuboresha maslahi na idaidi ya watumishi lengo likiwa na kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo wakati wa kufungua kikao kazi cha kujadili vifo vya kina mama na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi, kilichofanyika mjini hapa jana.
Alisema Serikali mkoani hapa imeendelea kujikita katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma ya afya kwa kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga vituo vipya vya kutolea huduma ,kununua vifaa tiba pamoja na gari la kusafirishia wagonjwa.
Muragili amebainisha kwamba vifo vya kina mama na watoto wachanga vimeendelea kupungua mkoani hapa kutoka vifo 55 mwaka 2016 mpaka 34 septemba 2021 wakati vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 701 mwaka 2016 mpaka kufikia vifo 508 septemba mwaka 2021.
Aidha Mulagiri ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kuhakikisha idadi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinaendelea kupungu ikiwezekana vimalizike kabisa kwa kuwa serikali imeanza kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya.
“Takwimu zinaonesha kwamba bado kazi kubwa inahitajika katika kukabiliana na matatizo yanayojitokeza wakati wa ujauzito,wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua kwa kuwa bado namba ya wanofariki ni kubwa sana”, alisistiza.
Aidha amesisitiza kwamba wataalamu wa afya kuendelea kuelimisha jamii kuhusiana na lishe bora wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua kama hatua ya kuboresha afya ya mama na mtoto na kuepuka vifo visivyokuwa vya lazima.
Amesema swala la afya ni la watu wote kwenye famililia hiyo kuwataka wanaume kushiriki kikamilifu katika huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kusaidiana na weza wao katika kuyakumbuka maamrisho na makatazo kwa wajawazito.
Hata hivyo Mulagiri amebainisha sababu za kutokea kwa vifo vya akina mama na watoto wachanga kwamba zipo huduma zinazotolewa kwa wakina mama wajawazito ambazo hazikizi viwango kulinga na miongozo mbalimbali ya huduma ya afya.
“Kukosekana kwa elimu ya uzazi kwa baadhi ya watu imekuwa ni moja ya changamoto inayosababisha vifo kwa kina mama na watoto wachanga” alisema Mhandisi Muragili.
Mulagiri ameitaka jamii kuachana na tamaduni na mila potofu zinazo wasababishia kutohudhuria kliniki, kufanya kazi zenye shuruba kwa muda mrefu na kuamini kwamba baadhi ya vyakula hawatakiwi kula kwa Imani wanayoijua wao wenyewe.
Akimalizia hotuba yake Mhandisi Muragili alivitaka vituo vya kutolea huduma kwa wazazi na watoto chini ya miaka mitano kuhakikisha huduma hizo zinatolewa bure kulingana na sera ya nchi inavyoelekeza na kuzitaka Halmashauri kusimamia hilo.
Mkurungezi Mtendaji Halmashauri ya Singida Vijijini Ester Chaula akimkaribisha mkuu wa wilaya alisema kwamba wataalamu hao wanakutana kila baada ya miezi mitatu ili kufanya tathmini ya hali ya kiafya mkoani humo zaidi kwa akina mama wajawazito na watoto.
Alisema kwamba katika Halmashauri hiyo wanaendelea kutoa chanjo mbalimbali kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ikiwa ni hatua muhimu ya kupambana na vifo vya watoto na wanawake wajawazito.
Awali Dkt.Erinest Mugetta Akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa alisema lengo la kikao hicho ni kupitia mikakati na maazimio ya kikao kilichopita na kuona namna ya utekelezaji wake na changamoto zilizotokea.
Alisema kikao hicho pia kililenga kuweka mikakati na maazimio mapya baada ya kutathimini afya ya uzazi na mtoto pamoja na vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua..
Ni wajibu wa kikao hicho kutathmini idadi ya vifo vya akina mama na watoto namna vilivyotokea na sabababu zilizosababisha kutokea alifafanua Dkt. Mugetta.
Kikao hicho kilihudhuriwa na madaktari bingwa wa watoto na akina mama, waganga wafawidhi kutoka Hospitali mbalimbali, mganga mkuu wa mkoa pampoja na waganga wakuu wa wilaya.