Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kipindi cha Mwezi wa Julai hadi Septemba 2021 ikiwa ni robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/22
……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu ametoa ripoti ya ukusanyaji wa mapato kwa robo ya mwaka katika halmashauri huku akiwaonya wakurugenzi ambao halmashauri zao zimefanya vibaya na wale wasiotekeleza maagizo hasa ya kutenga fedha za miradi ya maendeleo.
Wakati akitoa ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari Jijini Dodoma Waziri Ummy amesema kwa robo ya kwanza toka July hadi Septemba 2021 halmashauri zimekusanya zaidi ya bilioni 212.7 kati ya makadirio ya kukusanya bilioni 863.9 kwa mwaka 2021/2022.
Licha ya kufikia lengo bado kuna halmashauri zimefanya vibaya kwa kukusanya chini ya lengo na wengine wamefikia lengo lakini kuna kasoro katika kutekeleza maagizo ya kutenga fedha za maendeleo na asilimia 10 kwa makundi ya wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
“Kuna halmashauri 3 zimekusanya chini ya kiwango ambazo ni Tandahimba 3%, Nanyamba 6%, na Newala 8% lakini pia kuna baadhi ya halmashauri hazikupeleka fedha katika miradi ya maendeleo,
Pia wakurugenzi wa Halmashauri zote wajue kuwa wapo kwenye uangalizi wa miezi sita na miezi mitatu hii, kuna mingine mitatu baada ya hapo wale ambao hawatabadilika tutawapeleka katika ngazi za uteuzi na kwa hili hatuogopi kuitwa wanoko ” amesema.
Kuhusu hali ya ukusanyaji wa mapato amelitaja Jiji la Arusha kuwa limeongoza kwenye orodha ya majiji yaliyokusanya mapato mengi kwenye robo ya kwanza ya mwaka wa fedha kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio ya mwaka.
Kwa upande wa Mikoa iliyoongoza kwa ukusanyaji wa mapato, Mkoa wa Manyara umeongoza kwa kufikisha asilimia 40 ya makisio yake ya mwaka huku Mkoa wa Dodoma ukishika mkia kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio yake ambapo ametaka mikoa ambayo imefanya vibaya ijitathmini.
” Kwenye eneo la Halmashauri za Manispaa, kinara wa kundi hili ni Manispaa ya Kahama iliyokusanya asilimia 34 ya makisio yake ya mwaka, Bukoba asilimia 32, Mpanda asilimia 29 wakati Manispaa ya Mtwara ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya asilimia 15 kwenye kundi hili.
Kwenye kundi la Halmashauri za Miji, kinara ni Halmashauri ya Mji wa Mbulu ambao umekusanya asilimia 44 ya makisio yake ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Kibaha asilimia 43, Tunduma asilimia 39 wakati Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekua ya mwisho kwenye kundi hili ikikusanya asilimia 6,” Amesema Waziri Ummy.
Katika kundi la Halmashauri za Wilaya kinara wa kundi hilo ni Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ambayo imekusanya asilimia 66, Mlele, Meatu na Ngara wakikusanya asilimia 51 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba imekua ya mwisho katika kundi hili ikikusanya asilimia 3 ya makisio yake ya mwaka.
Waziri Ummy amesema uchambuzi wa taarifa hiyo ya ukusanyaji mapato katika robo ya kwanza unaonesha kuwa Halmashauri tano zimekusanya kwa asilimia 50 au zaidi ya lengo la mwaka wakati Halmashauri 47 zimekusanya kati ya asilimia 30 hadi 49.
Halmashauri 92 zenyewe zimekusanya kati ya asilimia 20 hadi 29 wakati Halmashauri 37 zimekusanya kati ya asilimia 10 hadi 19 na Halmashauri tatu zimekusanya chini ya asilimia 10 na hiyo ni kwa kuzingatia lengo la mwaka.