Na Joseph Lyimo
WATOTO wa jamii ya pembezoni wa wafugaji na wakulima wa Kijiji cha
Naepo, Kata ya Naisinyai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
wamenufaika na ujenzi wa shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza
aliyoijenga mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Bilionea Saniniu
Laizer.
Awali, wanafunzi hao iliwabidi watembee umbali wa kilomita tano kwenda
shule na kilomita tano kurudi nyumbani kwao.
Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo, Elia Daniel amesema anamshukuru
bilionea Laizer kwa kuwajengea shule hiyo hivyo kuwapa urahisi wa
kupata elimu.
“Tunamshukuru bilionea Laizer kwa kutujengea shule hii ambayo kwa
namna moja au nyingine itaturahisishia kupata elimu ya mchepuo wa
kiingereza kwa sisi wafugaji,” amesema.
Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite bilionea Saniniu Laizer,
amewahimiza Watoto wakike wa jamii ya kifugaji kusoma kwa bidii hadi
kufikia malengo yao ya kimaisha, badala ya kukimbilia kuozeshwa kimila
wakiwa na umri mdogo.
Pia, mdau huyo wa maendeleo amewataka wazazi wa jamii ya kifugaji
kuwapeleka watoto wao shule, badala ya kuwatumikisha katika kazi za
uchungi wa mifugo.
“Nalipongeza shirika la Elimisha Simanjiro Organization kwa kuweza
kuwasaidia watoto wetu ili waweze kusoma, jambo hili ni zuri ambalo
linapaswa kuigwa na kila mmoja wetu,” amesema bilionea Laizer.
Amesema akiwa miongoni mwa wadau wa elimu, jamii ya wafugaji mkoani
Manyara wanatakiwa kuitumia fursa iliyotolewa na shirika la Elimisha
Simanjiro Organization kwa kuwapeleka watoto wao shule badala ya
kuwatumikisha katika kazi za uchungaji wa mifugo.
“Wazazi hatuna budi kuwapeleka watoto wetu shule, tuacheni tabia ya
kuwaachia makundi makubwa ya mifugo ambayo mara nyingi huwashinda
nguvu na kusababisha migogoro kati yetu na wakulima” amesema Laizer.
Amesema ndiyo sababu akajenga shule hiyo ili Watoto wa pembezoni wa
jamii ya wafugaji na wakulima waweze kunufaika na elimu katika shule
hiyo ya mchepuo wa kiingereza ambayo ameikabidhi kwa serikali.
“Hakuna kitu kibaya sana kama kukosa elimu na katika karne hii ya 21,
hatutarajii kusikia kwamba kuna mzazi ameshindwa kumpeleka mtoto wake
shule eti kwa sababu ya kukosa ada kutokana na serikali yetu
inavyofanya” amesema bilionea Laizer.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Serera amempongeza bilionea
Laizer kwa kujenga shule hiyo ya mchepuo wa kiingereza ambayo
ameikabidhi serikalini kwa manufaa ya wanafunzi wa eneo hilo.
“Nakupongeza bilionea Laizer kwa kujenga shule hii kwani utaacha jina
na kumbukumbu ya maisha kuliko ungefanya jambo lingine la kifamilia
ila kwa suala la ujenzi wa shule na kuikabidhi serikali umefanya
kitendo kizuri mno,” amesema Dkt Serera.
Ofisa elimu msingi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Silvanus
Tairo amesema shule hiyo ni pekee ya serikali ya mchepuo wa kiingereza
kwenye wilaya hiyo kwani hakuna shule nyingine zaidi ya binafsi zenye
mchepuo wa kiingereza.
“Shule hii ilianza kama shule shikizi ila bilionea Laizer akaiboresha
kwa lengo la kuwasaidia Watoto wa eneo hili wasitembee umbali mrefu
kwa ajili ya kusoma elimu ya msingi ila hivi sasa imekuwa shule ya
mfano,” amesema Tairo.
Katibu mtendaji wa shirika la ESO Lowassa Edward Lekor, amempongeza
bilionea Laizer kwa kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ya mchepuo wa
kiingereza kwani itakuwa chachu ya mafanikio kwa jamii ya wafugaji wa
Tarafa ya Moipo.
Amesema umefika wakati watoto wa jamii ya kifugaji kutambua umuhimu wa
elimu na kila mmoja anafikia malengo aliyojiwekea hatimaye kuweza
kujiajiri yeye mwenyewe wakati atakapomaliza elimu yake ya juu hivyo
wanafunzi wachangamkie fursa hiyo.
Amesema kitendo cha ujenzi wa shule aliyofanya bilionea Laizer itakuwa
faida kwa jamii hiyo kwani elimu huwa inakwenda moja kwa moja kuwagusa
na kutetea haki ya kila mtoto kupata elimu bora na stahiki kuanzia
elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
Amesema wapo wanafunzi wa kiume wanaotoka katika jamii za kifugaji
wanakumbana na changamoto mbalimbali zinazochangiwa na baadhi ya mila
potofu zisizo rafiki na elimu zijukanazo kama Osingolio na Esoto.
“Hali hii imekuwa ikiwaathiri wale ambao wamekwenda jando kwa taratibu
za kimila na wengi wao wanajikuta kuacha masomo na kujiingiza kwenye
utafutaji wakiwa
na umri mdogo huku watoto wa kike wakiozeshwa hivyo wakipata shule
kama hii ya bilionea Laizer inakuwa nafuu,” amesema.
Mwenyekiti wa shirika la Elimisha Simanjro Organization (E.S.O)
Mwalimu Sooba Munderei Ngong’wa, amepongeza jitihada za dhati za
bilionea Laizer za kuunyanyua elimu kwenye tarafa ya Moipo kwa kujenga
shule hiyo ya mchepuo wa kiingereza.
Mwalimu Ngong’wa amesema bilionea Laizer anafanya kama shirika lao
lilivyolenga kuwasaidia watoto wa jamii ya kifugaji kuweza kupata
elimu ili na wao waweze kutimiza ndoto zao
kama ambavyo walivyo watoto wengine.
“Laizer amefanya jambo jema sawa na kampeni yetu ambayo imelenga
kwenda kuisaidia jamii ya kifugaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo
masuala ya elimu, ili kuweza kutokomeza ziro mashuleni, mimba za
utotoni, afya na mazingira,” amesema Mwalimu Ngong’wa.
“Tunatambua kwamba zipo changamoto nyingi katika jamii, wapo wazazi wanapenda
watoto wao wasome lakini unakuta mtoto mwenyewe hataki kusoma, sasa kupitia
kampeni hii ya ‘Niache Nisome’ tutawapitia majumbani mwao na
kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kupata elimu,” amesema.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian ametoa wito kwa serikali
kumsaidia mfadhili huyo kujenga bweni ili wanafunzi waweze kulala hapo
kwenye shule hiyo ya msingi ya bilionea Laizer ya mchepuo wa
kiingereza.
“Halmashauri inapaswa kumuunga mkono bilionea Laizer kwa kujenga bweni
kwani hivi sasa anataka kujenga bwalo la kula chakula kwa wanafunzi wa
shule hiyo hivyo aungwe mkono kwa serikali kuweka nguvu yake,” alisema
Taiko.