Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Omary Sukari,akizungumza
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya Mlele Rachel Kasanda, katikati ni Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera katika uzinduzi wa mfuko wa CHF iliyoboreshwa
Mkuu wa Mkoa wa katavi Juma Homera akikabidhi baiskeli kwa mmoja wa Waandikishaji wa Mfuko aliyefanya vizuri katika Halmashauri ya Mpimbwe
………………..
Na mwandishi wetu Katavi
Jumla ya kaya 1009 zenye wategemezi 4436 zimejiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii CHF iliyoboreshwa mkoani Katavi kwa lengo la kuwasaidia kurahisisha huduma za matibabu na kuepuka adha ya kutibiwa kwa waganga wa jadi kutokana na kushindwa kwenda kutibiwa hospitali kwa kuhofia gharama kubwa za matibabu
Wakizungumza katika uzinduzi wa Mfuko huo uliofanyika katika Kata ya Maji Moto katika Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele; baadhi ya wananchi waliojiunga na mfuko huo wamesema sasa wana uwezo wa kupata matibabu bure
Bwana Masalu Kafula ni mmoja wa wakazi wa Maji Moto ambaye amekata Bima hiyo na kuanza kuitumia, alisema inamsaidia yeye na familia yake kutowaza fedha za matibabu pale wanapougua
Akitoa taarifa katika uzinduzi huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dokta Omary Sukari amesema mkoa ulianza utekelezaji wa mfuko huo mwezi Juni mwaka huu
Aliongeza kuwa wananchi wameendelea kujitokeza kujiunga na mfuko huo tangu kuanza kwa utekelezaji wake mkoani hapa
“Hata hivyo niendelee kuwasihi wananchi kujiunga na mfuko huu, kwani tumeshuhudia watu wakiwatelekeza wapendwa wao hospitali kwa kushindwa kulipa gharama za matibabu” alisema Dk. Sukari
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi bwana Juma Homera alisema dhamira ya serikali ni pamoja na kuwaona wananchi wakiwa na afya bora
Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda alikuwa ni mmoja wa waalikwa katika hafla hiyo ambaye naye alitoa wito kwa wananchi kujiunga na mfuko huo
“Niwaambie ndugu sote ni wagonjwa watarajiwa, ni heri ukate Bima sasa ili usije ukaugua halafu ukasema ningelijua” alisema Pinda