Na Mwandishi Wetu, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge ameridhishwa na hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika nyanja za udhibiti, kasi ya ukusanyaji na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ambavyo vimewezesha kupaisha mapato kutoka 60.9 milioni mwezi Julai mwaka huu hadi kufikia milioni 139.3 mwezi Agosti.
Aidha, Dk. Mahenge amepongeza uamuzi wa halmashauri hiyo kutoa eneo la ekari 50 kwa Amcos ya wazalishaji zao la Mkonge iliyopo Kata ya Mudida Kijiji cha Mpipiti, ambapo pamoja na mambo mengine, ameahidi kuhakikisha anawaunganisha kikamilifu na Bodi ya Mkonge nchini ili kuwawezesha kuanza kunufaika na bei ya soko.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanaainisha vyanzo vyote vya mapato na kuvifanyia tathmini ili kubaini kila chanzo kihaulisia kinapaswa kukusanya kiasi gani gani cha fedha, kuweka usimamizi na udhibiti madhabuti, lengo ni kuwezesha vyanzo husika kuanza kukusanya mapato kwa asilimia 100.
“Nimeridhika na taarifa yenu hasa ya mapato, kikubwa hapa kaeni tengenezeni timu fanyeni analysis ya uhalisia wa kila kinachofanyika na kukusanywa kwenye vyanzo vyote rasmi na visivyo rasmi…tuwe na shabaha kwa kila tunachokifanya,” alisema.
Kuhusu uzalishaji wa zao la mkonge ambalo baada ya kuoteshwa limeonesha kutoa matokeo chanya na ubora wa hali ya juu kwenye ardhi ya Mkoa wa Singida, hususani ndani ya halmashauri hiyo, Mkuu wa Mkoa aliwahamasisha wana-singida na watakaohitaji kuwekeza kuchangamkia fursa ya zao hilo ambalo uwekezaji wake hauhitaji nguvu kubwa lakini faida yake ni kubwa.
“Uzuri wa mkonge hauna changamoto yoyote ukishapanda basi wewe unasubiri kuvuna tu…hivyo unaweza kulima mkonge na wakati huohuo ukaendelea na kilimo chako cha mazao mengine. Na mkonge wetu wa singida umeonekana kuwa bora zaidi na kimbilio kuliko maeneo mengine nchini,” alisema.
Katika hilo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba kwa sasa wakulima wa wilaya hiyo wanaozalisha mkonge wanapata tabu kubwa kutokana kulazimika kuuza kwa madalali ambao huwalangua, hivyo alipendekeza waanze kuuza kwa bodi ili kupata bei ya soko sambamba na halmashauri kupata mapato halisi na hatimaye wawekezaji wengi waweze kuja.
Pia katika hatua nyingine kupitia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elia Digha alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa namna alivyoonesha kuipenda na kuijali halmashauri kwa kuipatia shilingi bilioni cha 1.6 kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya elimu, afya na maji sanjari na fedha nyingine ambazo zimekuwa zikitolewa kwa kipindi tofauti kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Awali akizungumzia fedha hizo, pamoja na kumpongeza Rais Samia, Dk. Mahenge aliwaasa watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanazitumia fedha hizo kwa malengo kusudiwa.
“Niwasihi sana fedha hizo ni za moto…hazina posho wala urafiki. Hakikisheni kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa na kwa viwango na ubora stahiki,” alisema Mahenge.