Watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wanandoa, wamefariki dunia kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali katika maeneo mbalimbali ya mwili hadi kufa tukio lililotekelezwa katika wilaya ya Ludewa mkoani njombe.
Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa imeleza kuwa wanandoa waliouwawa ni Meniluph Ngailo na Mkewe Anes Ignas Haule ambapo wameuwawa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali katika eneo la shingo,kichwani na begani wakiwa nyumbani kwao
Kamanda Issah amesema hadi sasa jeshi linawashikilia wanandugu wawili kike na kiume ambao ni Nuru Ngailo na Everinjista Ngailo kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo huku imani za kishirikina zikitajwa kuhusishwa.
Mbali na tukio hilo katika mkoa huo ,Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imewahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa watano baada ya kukutwa na hatia ya kutekeleza mauaji.
Hukumu hiyo imesomwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Jose Mlyambina na katika mashitaka matatu ya mauaji aliyoendesha, shauri namba namba 56 ya mwaka 2016 ambalo washitakiwa Shaibu Putika(37) na Christopher Kahewanga(41) wote kwa pamoja wametiwa hatiani kwa kushiriki kutenda kosa la mauajii ya Chance Putika kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu Marejeo ya 2019.
Tukio hilo linatajwa kutendeka Mei 15, 2016 katika Kijiji cha Peruhanda kilichopo Wilaya na Mkoa wa Njombe .
Jaji Mlyambina ameeleza kuwa Mshtakiwa wa kwanza Shaibu Putika alimtafuta mshtakiwa wa pili Christopher Kahewanga ambaye walikubaliana kumlipa Tsh. laki tatu ili kutekeleza mauaji ya Chance Putika ambaye ni mdogo wa Shaibu Putika anadaiwa kuwa na tatizo ya akili.
Shauri lingine ni Shauri namba 53/2017, Mahakama Kuu kand ya Iringa kupitia Jaji Jose Mlyammbina imewahukumu washitakiwa watatu kunyongwa hadi kufa ambao ni Athony Magehema (28) Titho Nzota (34) na Emmanuel Magehema (27) baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Hilda Kinanilo katika kijiji cha Igominyi wilaya ya Njombe kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Tukio hilo limetajwa kutendeka marchi 28, 2016 katika Kijiji cha Igominyi wilayani Njombe ambapo washitakiwa wanadaiwa kumuua kwa kumchoma moto Hilda Kinanilo wakitumia mafuta ya petroli.
Mawakili wa serikali Matiku Nyangero na Andrew Mandwa wameieleza mahakama kuwa washtakiwa walimfuata Hilda Kinanilo nyumbani akiwa na mume wake na kuanza kuwakimbiza, ambapo mumewe Angelius Mayemba alifanikiwa kukimbia lakini mkewe Hilda Kinanilo alikamatwa na washitakiwa hao na kisha kumchoma moto hadi umauti.