*******************************
Na Joseph Lyimo
Wanawake mangariba wa jamii ya watadoga na wanyaturu wanaojishughulisha na ukeketaji kwenye Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, wameachana na ukeketaji na kujiunga na ujasiriamali.
Mangariba hao wamegeukia ujasiriamali wa kufanya shughuli za utunzaji wa ng’ombe wa maziwa, ufugaji nyuki na kuachana na ukeketaji waliokuwa wanawafanyia wasichana.
Wanawake hao wa vikundi vya ujasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji nyuki na utunzaji wa ng’ombe wa maziwa, vinavyofadhiliwa na Shirika la Oxfam na kuratibiwa na Shirika la Ujamaa la UCRT.
Mmoja wa wanawake hao mangariba, Pascalina Michael amesema mbali na vita inayopigwa na Serikali juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini vinaendelea hivyo wameamua kuachana navyo.
Pascalina amesema kutokana na Serikali kuvalia njuga suala la kuwakeketa mabinti wameonelea kuachana nalo na kugeukia ujasiriamali japokuwa hivi sasa wamebakia baadhi ya mangariba wanaowakeketa watoto wakiwa wadogo.
“Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyapaa imekuwa mkombozi kwetu wanawake lakini tunaiomba Serikali ielekeze nguvu hii katika kuwakagua watoto wanapokwenda kutibiwa au kliniki kwani vitendo vya ukeketaji vinafanywa na sasa ni kwa watoto wachanga si kwa wakubwa tena,” amesema.
Ngariba mwingine Tatu Abdalah amesema yeye awali alikuwa anaishi Singida na kuhamia Wilayani Hanang’ ambapo alikuwa anajihusisha na ukeketaji wa wasichana wa maeneo hayo.
Tatu amesema kutokana na miangaiko yake na vikwazo vya serikali ameamua kuachana na matukio ya ukeketaji na kujishughulisha na ujasiriamali ili ajiingizie kipato.
“Mangariba wengi wanafanya kazi ya kukeketa watoto wa watu kwa sababu ya kupata kipato ila kwa sababu hivi sasa serikali imeingilia hili jambo kwa nguvu kubwa tumeamua kutupa nyembe chini,” amesema Tatu.
Amesema utekelezaji wa mradi huo wa ufugaji nyuki katika kikundi chao umekuwa na changamoto katika kuwaletea mafanikio kutokana na uhaba wa maji.
Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iwawezeshe wachimbe bwawa kwa ajili ya kupata maji ya uhakika, kwani wanatembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo ya maji.
Ofisa wa maendeleo ya jamii wa wilaya ya Hanang’, Sarah Erasto amesema vita vya ukatili wa kijinsia kwa mwanamke vinaanza kwa wanawake wenyewe.
“Hakuna mwanaume anakuja kukeketa mwanamke ni ninyi wenyewe, lakini pia ndoa za utotoni na vipigo tuanze kukataa sisi kwanza kwa kujiunga katika vikundi kama hivi vya kuinuana kiuchumi” amesema Sarah.
Amesema unyanyapaa unaanzia pale mwanamke anapokuwa hana mchango katika jamii, lakini kumiliki uchumi unasaidia katika kupata heshima tofauti na hapo awali.
Amesema amefurahishwa na vikundi vya wanawake hao waliofadhiliwa na Oxfam kwa lengo la kuwakomboa katika mateso ya ukatili na unyanyapaa.
“Hilo la ukeketaji nitatafuta muda wa kuzungumza na wanawake peke yao, ila kwa sasa wanawake wenzangu chukueni silaha za vita dhidi ya ukatili na silaha hizo ni miradi ya kuwainua kiuchumi,” alisema Sarah.