Winga Zawadi Sanga wa timu ya Wizara ya Elimu (6) akikokota mpira dhidi ya wapinzani wake timu ya Wizara ya Madini ambapo walitoka suluhu katika michuano ya michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mchezaji Ester Turuka wa timu ya RAS Ruvuma akidaka mpira katika mchezo wa netiboli dhidi ya Tamisemi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, ambapo Tamisemi waliibuka kidedea kwa kufunga magoli 50-5 katika michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
Waamuzi wa mchezo wa netiboli wakifuatilia kwa makini matukio mbalimbali katika mchezo dhidi ya NFRA na Wizara ya Kilimo uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri, ambapo NFRA walifungwa magoli 37-28 katika michuano ya Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI).
Timu ya wanaume ya mchezo wa kuvuta Kamba ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo (kushoto) wakivutana na Mahakama katika michezo ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Mahakama walishinda kwa mivuto 2-0.
Timu ya wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba ya Mahakama (kushoto) wakiwavuta Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
*******************************
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TIMU ya Ofisi ya Rais Ikulu imewaadhibu bila huruma timu ya Wizara ya Madini kwa kuwafunga magoli 62-3 katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Ikulu inayoongozwa na wachezaji wazoefu na wakongwe waliwapeleka puta wapinzani wao, ambapo hadi mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 31-1.
Katika mchezo mwingine wa netiboli timu ya Ukaguzi waliwafunga timu ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa magoli 38-11. Washindi walikuwa mbele kwa magoli 20-4.
Nayo timu ya netiboli ya Wizara ya Mifugo iliwacharaza Maliasili na Utalii kwa kuwafunga magoli 27-1. Hadi mapumziko washindi waliongoza kwa magoli 13-0. Nayo Tamisemi waliwacharaza RAS Ruvuma kwa magoli 50-5. Washindi walikwenda maoumziko kwa magoli 21-1.
Mchezo mwingine ni timu ya NFRA ilifungwa na Wizara ya Kilimo kwa kuwafunga magoli 37-28. Hata hivyo hadi mapumziko Kilimo walikuwa wakiongoza kwa magoli 18-16. Nayo timu ya Katiba na Sheria waliwafunga Tume ya Uchaguzi kwa magoli 22-16.
Kwa upande wa soka mabingwa watetezi timu ya Wizara ya Elimu walitoka suluhu na Wizara ya Madini katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri. Nayo timu ya Waziri Mkuu waliwafunga Wizara ya Afya kwa goli 1-0.
Nayo Ukaguzi waliwaadabisha Wizara ya Maji kwa kuwafunga magoli 5-2 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Morogoro. Magoli ya washindi yalifungwa na Aboubakar Kilimo, Henry Sempa, Peter Tinno, Khalid Pandawe na Masoud Suleiman; huku magoli ya Maji yalifungwa na Raphael Mkumba na Omari Gumbo.
Katika mchezo mwingine wa soka timu ya Wizara ya Mifugo iliwashinda Hazina kwa bao 1-0 lililofungwa kwa njia ya penati na Jumanne Bunju baada ya kipa Ramadhani Abdulwahadi kumchezea rafu Nkana Eliud katika eneo laa hatari.
Nazo timu za mchezo wa kuvuta kamba za Mahakama kwa wanaume na wanawake zimewavuta Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mivuto 2-0.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za netiboli kati ya Wizara ya Maji kuumana na Ikulu huku Wizara ya Viwanda watakutana na Mahakama; wakati katika mchezo wa kuvuta Kamba kwa wanawake timu ya Uchukuzi watacheza na Kilimo, nao wanaume timu ya Uchukuzi wataumana na RAS Ruvuma.
Katika mchezo wa soka timu ya Kilimo watakutana na Maliasili na Utalii; huku Mahakama watapepetana na RAS Morogoro.