Na Joseph Lyimo
MKUU wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Janeth Mayanja, amesema wananchi wa eneo hilo wamemaliza dozi 2,050 za dozi za chanjo za Uviko-19 aina ya Janssen (Johnson & Johnson) zilizotolewa na Serikali.
Mayanja akielezea mafanikio ya chanjo ya Uviko-19 amesema wao kama Wilaya Agosti 3 mwaka huu walipokea dozi 1,000 za chanjo aina ya Janssen (Johnson & Johnson).
Mkuu huyo wa wilaya ya Hanang’ amesema Septemba 21 mwaka huu waliongezewa tena dozi nyingine 1,000 za aina hiyo hiyo ya Janssen.
“Mwezi huu wa Oktaba 11 tuliongezewa tena dozi nyingine 50 za chanjo ya Uviko-19 za aina hiyo hiyo ya Janssen nazo zimekwisha hivyo kufikisha jumla ya chanjo zote kuwa 2,050” amesema.
Amesema kamati ya usalama ya wilaya hiyo ilizindua shughuli ya kupata chanjo Agosti 5 mwaka huuu na awali chanjo ilikuwa inatolewa kwenye vituo vitatu ila baadae vituo viliongezwa hadi kufikia 25.
Amesema chanjo hizo zilisambazwa kwenye vituo 25 vya kutolea huduma ambavyo ni Gitting, Barjomot, Gendabi, Dawar, Bassotu, Getanuwas, Murjanda, Tumaini na Endasak.
Ametaja vituo vingine ni Katesh, Simbay, Waama, Waranga, Balangdalalu, Murumba, Nangwa, Dirma, Dumbeta, Gidahababieg, Sirop, Masakta, Bassodesh, Mulbadaw, Setchet na Gidagamowd.
“Uhamasishaji umefanyika katika taasisi za umma na binafsi na maeneo yenye mikusanyiko chanjo zilizotolewa ni 2045 na kubakiwa na chanjo tano ambazo zitamalizika wakati wowote hadi hivyo tumeomba chanjo zaidi,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema uhamasishaji unaendelea na amewashukuru viongozi wa dini, wazee maarufu, wadau,wakuu wa taasisi na wananchi wote kwa kufanikisha suala hilo.
Mmoja kati ya wakazi wa kata ya Simbay waliopata chanjo hiyo, John Kidangay amesema serikali iliwashirikisha wananchi na kuwaeleza faida ya chanjo hiyo ndiyo sababu wananchi wakashiriki kwa wingi.
“Wale waliokuwa wanapotosha walishindwa kufanikiwa kutokana na wao kutokuwa na hoja ya maana ndiyo sababu wananchi hawakuwasikiliza na kushiriki chanjo hiyo,” amesema Kidangay.
Mkazi wa kijiji cha Endasak, Erasto Elia amesema elimu iliyotolewa na wataalam wa afya imechangia wao kushiriki kikamilifu shughuli ya kupatiwa chanjo ya Uviko-19.
Elia amesema awali baadhi ya watu walizusha maneno ya potofu na kuwapa watu hofu kuwa chanjo hiyo ina matatizo kwa wananchi jambo ambalo siyo kweli.