……………………………………………………….
Na Asila Twaha – Morogoro
Timu ya TAMISEMI Queens yaichapa bila huruma timu ya Ras Ruvuma magoli 50- 4 katika Mashindano ya SHIMIWI.
Mchezo huo umechezwa mapema ambapo timu ziliingia uwanjani majira ya saa 1 asubuhi ikiwa ni michezo yao ya awali katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za serikali ambayo Kitaifa yanafanyika katika uwanja wa Jamhuri Morogoro Mjini.
Katika mchezo wa mpira wa pete TAMISEMI Queens wameonesha kiwango cha hali ya juu hii ikidhirishwa na ushindi walioupata hii leo.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku timu ya TAMISEMI Queens ikishambulia lango la timu ya Ras Ruvuma kama nyuki mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika TAMISEMI Queens ilikua mbele kwa magoli 21 dhidi ya timu ya Ras Ruvuma ikiambulia goli 1.
Katika kipindi cha pili mchezo huo uliendelea kuwaelemea Ruvuma ambapo kwa mara nyingine tena waliruhusu kupokea magoli 29 kwa 3 hivyo kuhitimisha mchezo huo kwa timu ya TAMISEMI Queens kuibuka na ushindi mnono wa magoli 50 kwa 4.
Flora Odilo wa timu ya TAMISEMI Queens alionekana kuwa nyota wa mchezo huo akiipatia timu yake magoli 30 na Dafrooza Luhwago akipachika magoli 20.
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo timu ya TAMISEMI Queens inatarajia kukutana na Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje kesho.