Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaji Majid Mwanga akitoa maelezo na maelekezo kwa Kamati ya Maliasili na viongozi wa Kijiji cha Kitunduweta, kata ya Muhenda kuhusu kuongeza juhudi za kulinda na kuhifadhi Msitu wa Matalawe, kulia kwa DC ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Wilfred Sumari na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Kisena Mabuba (Picha na Mpiga Picha wetu). Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Kisena Mabuba akijibu maswali ya baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitunduweta kata ya Muhenda wilayani humo.Kulia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Revocatus Njau na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga.
Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo akitoa ufafanuzi kuhusu Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ta Mkaa Tanzania mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaji Majid Mwanga na wananchi wa kijiji cha Kitunduweta kata ya Muhenda.
***********************************
Na Mwandishi Wetu
KAMATI za Maliasili za vijiji vinavyojihusisha na uhifadhi na uvunaji misitu kwa njia endelevu wilayani Kilosa mkoani Morogoro zimeagizwa zisikubali kuyumbishwa na viongozi kinyume na taratibu.
Maagizo hayo yametolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kitunduweta kata ya Muhenda baada ya kufanya ziara ya kuangalia shughuli za uhifadhi na uvunaji endelevu unaondelea katika misitu.
Alhaj Mwanga alisema kwa muda mchache ambao amekuwepo hapo kama mkuu wa wilaya amebaini kuwepo vitendo vya baadhi ya viongozi wa vijiji na kata kuingilia kamati za maliasili hali ambayo inaondoa ufanisi wa kamati hizo.
Alisema kamati za maliasili katika vijiji vyenye misitu zipo kisheria hivyo zinapaswa kuheshimiwa ili zifanye kazi kwa weledi na uaminifu kwani kinyume chake watachangia upotevu wa rasilimali misitu.
Alisema taarifa alizo nazo kuhusu Kamati ya Maliasili ya Kitunduweta kumekuwepo na baadhi ya viongozi kuingilia jambo ambalo hatakuwa tayari kuliruhusu.
“Nina taarifa kuwa Katibu wa Kamati ya Maliasili Kitunduweta anataka kujiuzulu kwa sababu ya viongozi wanaingilia majukumu yenu, mimi nipo na nyie kazeni mguu na kama itatokea tena anawapa maagizo nipeni taarifa nitamshughulikia,” alisema.
Alhaj Mwanga alisema kamati hiyo imefanya kazi nzuri ya kulinda misitu katika kijiji hicho hivyo inapaswa kuungwa mkono ili kuhakikisha sumu hii ya kuhifadhi misitu inafika kila mahali wilayani Kilosa.
Mwanga aliitaka kamati hiyo kutafakari na kufanya mabadiliko iwapo itaona inafaa ili kuhakikisha wanakuwa na watu sahihi wasiokengeuka.
Mkuu huyo wa wilaya alisema uwekezaji uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usisimamizi wa Misutu Tanzania (MJUMITA) kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) unapaswa kuungwa mkono kwa kuhakikisha misitu inakuwa endelevu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilosa Wilfred Sumari, alisema halmashauri itawapa ushirikiano wananchi wote ambao wanasimamia rasilimali misitu kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo na uchumi.
Sumari alisema hali ya uharibifu wa misitu katika maeneo ambayo hayana miradi ni mbaya hivyo kuwataka wananchi wote kuwa mabalozi wa uhifadhi ili misitu kuwa endelevu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Kisena Mabuba alisema halmashauri haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi yoyote ambaye atabainika kushiriki kuhujumu rasilimali misitu ambayo ni muhimu kwa nchi.
“Yamesemwa mengi na wananchi ofisi yangu itafuatilia iwapo itabaini ushiriki wa mtumishi wa umma haitasita kuchukua hatua ili kuhakikisha misitu inakuna salama,” alisema.
Mabuba aliwaagiza makatibu tarafa na watendaji wa kata, vijiji na vitongoji kuhakikisha wanatatua changamoto zilizopo katika ngazi zao hasa katika eneo hilo la uhifadhi wa misitu hali ambayo itachangia rasilimali hiyo kuwa endelevu.
Katibu wa Kamati ya Maliasili Kijiji cha Kitunduweta, Leoti Msoloka alisema hali ya uhifadhi katika kijiji chao ni nzuri huku akitoa rai kwa watendaji wa vijiji kuacha kuingilia majuku yao hali inayowakatisha tamaa kulinda rasilimali hiyo adimu.
Msoloka alisema changamoto kubwa katika uhifadhi wa misitu ni moto na mifugo jambo ambalo linawakatisha tamaa hasa ikizingatiwa kuwa wapo viongozi wanatajwa kushiriki.
Mnufaika wa Mradi wa Usimamizi Shiriki wa Misitu ya Jamii (USMJ), kupitia uchomaji mkaa, Kulangwa Ganda alisema ujio wa mradi huo umeweza kubadilisha maisha yake na kijiji kwa ujumla.
Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema ushiriki wa halmashauri katika uhifadhi utaongeza motisha kwa wananchi wanaozungukwa na rasilimali hiyo kuipenda na kuitunza.
“Sisi TFCG tulichokifanya ni kuleta mtoto na kumlea hadi amekuwa hivi sasa tumeshatoa mguu mmoja nje mwaka 2022 tunatoa wa pili imani yetu ni kuona baada ya kutoka kabisa mtoto huyu anahudumia familia yake mwenyewe bila kutegemea mtu mwingine,” alisema.