Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa kuzindua kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Gerald Mweli akizungumza wakati wa uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari vitakavyosambazwa katika halmashauri zote nchini.
Kulia nia Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo na kushoto ni Gerald Mweli Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) na viongozi wengine wa Elimu, wakionesha vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari vitakavyosambazwa katika halmashauri zote nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) Katibu Mkuu Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Gerald Mweli wakikagua moja ya kitabu wakati wa uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akigawa vitabu kwa mmoja wa wanafunzi walioshiriki hafla ya uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari iliyofanyika Jijini Dar es Salaam
Muonekano wa baadhi ya vitabu vya kiada vitakavyosambazwa kwenye halmashauri zote nchini ili viweze kutumika shuleni.
………………………………………………………………….
•Zaidi nakala milioni 20 kusambazwa
•Zaidi ya Shilingi bilioni 46 zimewezesha uandishi, uchapaji na usambazaji
•Ataka maafisa Elimu kuhakikisha vinafika shuleni na kutumika
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewaagiza maafisa elimu wote wa ngazi za Halmashauri kuhakiksha wasimamia usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari ili vifike shuleni kwa wakati na kutumika ili malengo ya Serikali ya kuwapatia elimu bora watoto wa kitanzania yaweze kutimia.
Waziri Ndalichako amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu hivyo vilivyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambapo amesema vitabu vya kiada ni nyenzo muhimu katika kutekeleza dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji kwani humrahisishia mwanafunzi kuweza kufuatilia yale yanayofundishwa, kujisomea wenyewe lakini pia yanamuongoza mwalimu katika utekelezaji wa jukumu zima la ufundishaji.
Waziri Ndalichako amesema vitabu ambavyo vimeandaliwa vimelenga kwa shule za aina zote zinazotumia lugha ya Kiswahili na kingereza na kwamba vitabu vya kiada kwa shule za msingi vitapelekwa kwenye halmashauri zote 184 za mikoa yote ya Tanzania bara kwa uwiano wa kitabu kimoja wanafunzi wawili huku vile vya sekondari vikigawiwa kwa upande wa Bara na Zanzibar.
Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na washirika wa maendeleo kwenye Sekta ya Elimu ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau hao imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 46 zilizowezesha uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari nakala milioni 20,943,989.
“Wanasema ukiona vyaelea jua vimeundwa. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu ametuwezesha Wizara kutoa machapisho haya, tungewezaje kutoa nakala zote hizi bila kuwezeshwa, naahidi tutaendelea kusimamia kila fedha inayokuja kwa ajili ya kuendeleza elimu ya watanzania ,” amesema Waziri Ndalichako
Amemshukuru mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Jenerali Venance Mabeyo kwa kuendela kutoa ushirikiano kwa Wizara anayoisimamia katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo hili la kutoa magari kwa ajili ya usambazaji wa vitabu vya kiada kwa shule ya Msingi na sekondari.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema wizara itaendelea kuisaidia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambayo iko chini ya Wizara ili kuhakikisha inatekeleza majukumu kwa ufanisi kwani inasimamia majukumu yote kuandaa mitaala, mihtasari katika ngazi ya elimumsingi.
Nae Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Gerald Mweli amemuahidi Waziri Ndalichako kuwa Vitabu hivyo pindi vitakapofika katika Halmashauri watahakikisha ndani ya wiki moja viwe vimefika shuleni na kuanza kutumika ili kutofifisha juhudi za Mhe. Rais za kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu iliyo bora.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba ametaja makundi ya vitabu vinavyoandaliwa kuwa ni vitabu vya kiada vya masomo yote ya madarasa ya Awali, Darasa la I-IV kwa shule zinazotumia lugha ya kingereza na kiswahili kufundishia, viongozi vya mwalimu I-VII, Mihtasari, viongozi vya mwalimu na vitabu vya wanafunzi walio nje ya mfumo rasmi kundirika la I mwaka wa I na wa II na vitabu vya kiada kidato cha I-IV
Kwa upande wa Sekondari vitabu vilivyoandaliwa ni kwa masomo ya Bailojia, Fizikia, Home Economics, Kiswahili, Civics, Kemia, ICs Mathematics, Jiografia, Historia, kingereza na Kilimo.