Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam walipomtembelea ofisini kwake kumtaarifu kuhusu kuanza kwa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo.
Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Bi. Honester Ndunguru akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge ofisini kwake kuhusu kuanza kwa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo.
Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Bi. Honester Ndunguru akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imeanza tarehe 13 na itamalizika tarehe 27 Oktoba, 2021 mkoani Ruvuma.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam Bi. Julieth Shehiza akifurahia jinsi mfanyabiashara wa Mjini Songea mkoani Ruvuma anavyotunza kumbukumbu zake za biashara vizuri wakati wa kampeni ya elimu kwa mliapakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam Bw. Godfrey Kumwembe akimuelimisha Bw. Hekima Kaduma ambaye ni mfanyabiashara wa duka la pembejeo mkoani Ruvuma kuhusu utumiaji sahihi wa mashine za EFD wakati wa kampeni ya elimu kwa mliapakodi inayoendelea mkoani humo.
(PICHA ZOTE NA TRA).
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge amewataka wananchi kuchangamkia kampeni ya elimu kwa mlipakodi ili kuongezea uelewa na uhiari wa kulipa kodi nchini.
Akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam walipomtembelea ofisini kwake mkoani Ruvuma kumtaarifu kuhusu kuanza kwa kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo ameeleza kuwa, huu ni muda muafaka wa walipakodi kuongeza uelewa wa masuala ya kodi ikiwa ni pamoja na kueleza changamoto zao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.
“Nimefurahia ujio wa kampeni hii hapa Mkoani kwangu hivyo napenda kuwahimiza walipakodi wote kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA wanaofanya zoezi hili ili waweze kujiongezea uelewa wa kodi lakini pia ni wakati muafaka wa kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa na hatimaye kuongeza uhiari wa kulipa kodi,” alisema Mhe. Mkuu wa Mkoa huyo.
Kwa upande wake Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Bi. Honester Ndunguru amesema lengo la kampeni hiyo ni kusogeza huduma karibu, kuwaelimisha walipakodi na kujenga urafiki kati ya TRA na walipakodi kwa ajili ya kuongeza ridhaa ya ulipaji kodi.
“Pamoja na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili walipakodi wetu lakini pia kampeni hii imelenga kutoa elimu, kusogeza huduma karibu kwa wateja wetu pamoja na kusajili walipakodi wapya ili kuongeza idadi ya walipakodi nchini na ridhaa ya kulipa kodi,” alisema Bi. Ndunguru.
Naye, Mfanyabiashara wa duka la nguo mkoani hapa Bw. Joseph Ngocho baada ya kupata elimu ya kodi wakati wa kampeni hiyo, amesema hii ni mara ya kwanza maofisa kutoka makao makuu kumtembelea ofisini kwake na kumuelimisha kuhusu umuhimu wa kulipa kodi hivyo ameomba zoezi hilo liwe endelevu.
Hekima Kaduma ni mfanyabiashara wa duka la pembejeo ambaye amesema kuwa, kampeni ya elimu kwa mlipakodi pamoja na kuwapatia elimu ya kodi lakini pia inasaidia kuondoa hofu ya kuwaogopa maofisa wa TRA maana walipakodi wanapata muda wa kuzungumza na kutoa changamoto zao tofauti na ofisini ambapo ni vigumu kupata fursa hiyo kutokana na wateja kuwa wengi.
“Kwa kweli naishukuru TRA kwa kutuletea kampeni hii maana inatupa muda wa kutosha wa kuelimishwa na sisi tunapata nafasi ya kutoa maoni na kero zetu tofauti na kusubiri kuwafuata ofisini ambapo unakuta wateja wengi lakini pia wakati mwingine tunapata woga wa kutoa dukuduku letu,” alisema Bw. Kaduma.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkaoni Ruvuma imeanza tarehe 13 na itamalizika tarehe 27 Oktoba, 2021 ikipita katika wilaya zote za mkoa huo ambazo ni Namtumbo, Mbinga, Songea, Nyasa na Tunduru.