Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Jimbo la Rorya Mkoani Mara, Japhary Chege Wambura, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulipatia jimbo hilo shilingi bilioni 13 za miradi mbalimbali maendeleo.
Mbunge Japhary ameyasema hayo kwenye ukumbi wa Kazamoyo Inn, (Kwa Luka) Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, wakati akizungumza na wananchi wenye asili ya Rorya wanaoishi mji mdogo wa Mirerani.
Amesema Rais Samia ametoa fedha hizo shilingi bilioni 13 ambazo zinafanikisha maendeleo ya wananchi wa jimbo la Rorya kwenye sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na maji.
Amesema hivi sasa uchaguzi umemalizika hivyo jamii ya Rorya inapaswa kuungana ili kufanikisha maendeleo kwenye jimbo hilo ambalo limegubikwa na wimbi la umasikini.
“Nawashukuru kwa moyo wa dhati kabisa kwani hivi sasa baada ya mimi kuchaguliwa ninapita kwenye kata zote za Jimbo la Rorya kwa ajili ya kuwashukuru na kusikiliza changamoto zao na ndugu zetu wengine waliopo Arusha na Mirerani,” amesema Japhary.
Amewaahidi wananchi wa jimbo la Rorya kuwatumikia kwa dhati ili kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili zinamalizika kama siyo kupungua ila yote yatatokana na ushirikiano wao.
Hata hivyo, amewapongeza na kuwashukuru wananchi wenye asili ya jimbo la Rorya, wanaoishi jijini Arusha na mji mdogo wa Mirerani kwa namna wanavyokumbuka nyumbani na kuchangia maendeleo ya jimbo la Rorya.
“Tunawashukuru mno na katika kufanikisha maendeleo ya wananchi wa jimbo la Rorya, tumebuni mpango wa kuchangia shilingi elfu mbili kwa kila mwezi ili kutunisha mfuko wa maendeleo,” amesema.
Amesema atakuwa anaisemea Rorya kwenye kila jambo ambalo halijakaa vizuri na hata bungeni huwa anazungumza kila mara pindi akiona hakuna fungu la kutosha lililopangiwa kwao.
Mwenyekiti wa Mara Group, Godwin Kosodo amempongeza mbunge huyo kwa namna anavyoshiriki kupambania maendeleo ya wananchi wa jimbo la Rorya na huwa wanamuona bungeni Dodoma anavyoizungumzia Rorya.
Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia, amesema wapo pamoja na Mbunge Japhary katika kumuunga mkono kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Rorya.