Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Italia katika Ubalozi wa Tanzania uliopo Roma,Italia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Italia pamoja na Watanzania wanaoishi nchini Italia.
……………………………………………………………….
Serikali imesema iko katika hatua ya uchambuzi wa maoni wa kukamilisha mchakato wa hadhi maalum kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kabla ya kuupeleka bungeni ili kuwawezesha kushiriki na kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi yao ya asili.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameitoa kauli hiyo Roma,Italia wakati akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio nchini humo na kutanabaisha kuwa tayari mchakato wa awali wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau wote wakiwemo diaspora umekamilika na sasa wataalamu wako katika hatua za uchambuzi wa maoni hayo
Balozi Mulamula ameongeza kuwa mchakato wa hadhi maalum utakapokamilika utatoa haki za kiraia kwa watanzania waishio nje ya nchi isipokuwa kushiriki katika siasa kwa kuwa suala hilo linahitaji mapitio ya kikatiba
Amewaeleza kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatambua mchango unaofanywa na diaspora katika kujitafutia maendeleo yao na kuwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa kushiriki katika kuijenga Tanzania kwa kuitangaza vyema kibiashara na kuleta wawekezaji katika sekta mbalimbali pamoja na kuleta ujuzi.
Akizungumza kwa niaba ya Watanzania waishio nchini Italia,Bi Anastazia Lubangula amesema wanaunga mkono hatua ya Serikali ya kuanzisha mchakato wa kuwapatia hadhi maalum kwa kuwa itawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kuaminiana.
Watanzania hao wameiomba Serikali kuangalia upya suala la kuwawezesha kufungua akaunti katika benki za Tanzania kwa kuwa sheria inayosimamia suala hilo inawanyima haki ya kujiwekea akiba nyumbani kupitia Benki lakini pia inainyima Serikali mapato.
Watanzania hao wametoa pongezi zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendesha shughuli za kiutawala tangu aingie madarakani miezi 6 iliyopita na kwamba wana imani uongozi wake utaondoa mikwamo na kuimarisha uhusiano na mataifa na Taasisi za Kimataifa kwa maendeleo ya Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula anahitimisha ziara yake nchini Italia ambapo ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Italia,Mkutano wa Kimataifa wa Amani pamoja na kukutana kwa mazungumzo na viongozi wa Taasisi za Kimataifa ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na Mfukowa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD)