****************
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ameishukuru serikali kwa uboreshwaji wa mindombinu ya Elimu katika Jimbo la Dodoma Mjini kwa kutekeleza miradi mbali mbali yenye lengo la kuweka mazingira rafiki ya usomaji.
Mavunde ameyasema hayo leo alipotembelea Shule ya Msingi Medeli iliyopo kata ya Tambukareli na kukagua ujenzi wa madarasa mapya,matundu ya vyoo,ukarabati wa madarasa ya zamani na uchimbaji wa kisima mradi unaogharamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania wa jumla ya Tsh 345 milioni.
“Ninaishukuru Serikali chini ya Rais Mh Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya Elimu.
Mwaka 2016 nilikuja katika shule hii na kukuta madarasa mengi hayafai na kuta zake kukaribia kudondoka,niliwaahidi kwamba kupitia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM tutaboresh mazingira ya shule na ninyi leo ni mashahidi wa namna ambavyo shule hii imebadilika ndani ya muda mfupi.
Na leo nitawanunulia seti 1 ya computer kwa ajili ya uchapishaji wa mitihani hapo shuleni ili tuwaandae vyema watoto wetu wenye mitihani ya mwisho ya Taifa”Alisema Mavunde
Akitoa salamu za Shule,Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Medeli Bi. Grace Risasi ameishukuru serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule ambao umepelekea kuongezeka kwa ufaulu katika shule hiyo kwakuwa mazingira ya ufundishaji na usomaji umekuwa rafiki tofauti na awali.