*****************************
Na Joseph Lyimo
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Manyara, (RAS) Catherine Mthapula amewataka wajumbe wa kamati ya maafa ya Mkoa huo, kuhamasisha jamii ya eneo hilo kupata chanjo ya Uviko-19 kwani ni chanjo salama.
Mthapula akizungumza na wajumbe wa kamati ya maafa wa Mkoa huo kwenye kikao kazi mjini Babati, amesema wajumbe hao wana nafasi kubwa ya kuhamasisha jamii kupata chanjo.
“Mnapaswa kuwa mabalozi wazuri kwenye suala hili la chanjo kwani Serikali imefanikiwa kusambaza chanjo kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa wetu hivyo jamii ishiriki kuchanja,” amesema Mthapula.
Amesema anatarajia wajumbe hao watafikisha taarifa hiyo kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya zao ili wananchi wa sehemu hizo washiriki kupata chanjo ya kupambana na janga la Uviko-19.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt Damas Kayera amesema kuanzia Agosti 3 mwaka huu, mkoa huo ulipokea dozi 15,000 ya chanjo ya Uviko-19 kwa ajili ya jamii ya eneo hilo.
Dkt Kayera amesema bado jamii ya Mkoa wa Manyara ina uelewa mdogo wa kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo kupambana na ugonjwa wa Uviko-19.
“Wataalamu mbalimbali wa mkoa wa Manyara wamejipanga kutoa elimu ya Uviko-19 ili wananchi wapate chanjo ya kupambana na janga hilo,” amesema Dkt Kayera.
Amesema hivi sasa dunia bado inakabiliwa na ugonjwa wa Uviko-19 ambao unapoteza maisha ya watu, hivyo wananchi wa Manyara wanapaswa kuchukua tahadhari ya janga hilo.
Mkazi wa Mjini Babati, John Matle amesema elimu ikitolewa kwa wananchi wa eneo hilo watafanikiwa kuelewa kuwa chanjo ya Uviko-19 haina tatizo hivyo jamii ishiriki kwa kuchanja.
“Baadhi ya watu wanaeleza mambo ambayo hayana msingi kuwa viongozi wa awamu ya tano waligoma chanjo isitumike ilihali walieleza kuwa utafiti ufanyike kwanza na umeshafanyika tatizo lipo wapi? Amehoji Matle.
Mkazi wa Wang’waray mjini Babati, Magreth Bombo amesema baada ya kupatiwa elimu ya chanjo hiyo aliamua kuchanja yeye na mke wake na watoto wake wawili wenye miaka 23 na 19.
“Chanjo tumepata mimi na familia yangu na hakuna tatizo lolote tulilolipata hivyo ni wakati wa wananchi wengine ambao hawajachanja wafanye hivyo,” amesema Bombo.