SIMBA SC imelazimisha sare ya bila kufungana na wenyeji, Uniao Desportiva do Songo, kifupi UD Songo katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo mjini Beira nchini Msumbiji.
Sasa Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems itakuwa na kibarua chepesi kidogo kwenye mchezo wa nyumbaji Jumapili ijayo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, ikihitahi ushindi wowote ili kusonga mbele.
Mchezo wa Simba SC ilionekana kabisa kusaka sare, kwani iliuanza kwa kucheza kwa kujihami zaidi, ikiweka vioungo wengi wa ulinzi.
Lakini robo ya mwisho kocha Aussems aliongeza nguvu kwenye safi ya ushambuliaji kwa kumtoa kiungo wa ulinzi, Jonas Mkude na kumuingiza kiungo mshambuliaji, Hassan Dilunga.
Lakini pia alimpumzisha kiungo wa zamani wa Gor Mahia ya kwao, Kenya na kumuingiza aliyekuwa winga wa TP Mazembe ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
UD Songo nao walifanya mabadiliko mawili, wakimtoa Mmalawi Frank Banda na Jose Silva Junior na kuwaingiza Mario Sebastiao Sinamunda na Stelio Ernesto.
Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Kikosi cha Simba Sc kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude/Hassan Diliunga dk78, Clatous Chama, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata/Deo Kanda dk71.