****************************
Na Joseph Lyimo
WAJUMBE wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamepatiwa elimu ya faida ya chanjo ya Uviko-19 na kutakiwa kuepuka maneno potofu yanayosemwa na kuepuka kupata juu ya chanjo hiyo.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Dkt Aristidy Raphael ametoa elimu hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani.
Dkt Raphael amesema viongozi hao wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani wanapaswa kushiriki kuchanja chanjo hiyo na kuepukana na maneno ya watu potofu.
“Chanjo hii ni salama kwani imepitishwa na shirika la afya duniani WHO na watanzania wakafanya utafiti na kuona inafaa kwa matumizi ya kupambana na Uviko-19,” amesema Dkt Raphael.
Amesema Julai 28 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan amethibitisha kwa wananchi kuwa chanjo hiyo haina madhara na akawa raia namba moja kwenye kuchanja ili kuonyesha mfano.
Amesema chanjo hiyo inasababisha kuwepo na kinga ya Uviko-19 kwenye mwili hivyo watanzania wachanje kwani ina uwezo mkubwa wa kupambana na kirusi hicho.
“Matibabu ya Covid-19 ni gharama kubwa wengine wanatumia hadi shilingi milioni saba na zaidi hivyo tushiriki hili kwani hata mimi nimechanja na sijapata madhara,” amesema Dkt Raphael.
Mwenyekiti wa mtaa wa Tupendane, Idd Abdi amehoji kuna mtu mmoja mara baada ya kupata chanjo ya Uviko-19 alieleza kuwa nguvu zake za kiume ziliongezeka.
Abdi akahoji kuwa mtu akipatiwa chanjo ya Uviko-19 ya Johnson and Johnson, endapo likija wimbi lingine atapata chanjo upya au itakabiliana nayo hiyo hiyo?
Katibu wa CCM kata ya Endiamtu, Anthon Jacob Mavili amesema yeye ni miongonni mwa watu waliopata chanjo ya Uviko-19 ila hajapatiwa cheti vya elektroniki kama maeneo mengine wanavyopewa.
Mjumbe wa viti maalum wa mamlaka ya mji huo, Jema Lilama amehoji juu ya umuhimu wa kujaza fomu na kuandika taarifa ya mtu kabla ya kupatiwa chanjo hiyo ya Uviko-19.
Mwenyekiti wa mtaa wa Manyara, Boazi Ambonya amesema idadi ya watu wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi huwa inabainishwa wazi kupitia takwimu zianazotolewa na Serikali kati ya idadi ya watanzania zaidi ya milioni 60 hivyo takwimu za wenye Uviko-19 iwe inatolewa kila mara.
“Hatupaswi kuficha idadi ya wenye Uviko-19 hivyo serikali iige mfano wake kwenye VVU huwa wanatoa takwimu kwa watu waliopata maambukizi hivyo wafanye hivyo pia kwenye janga hili,” amesema Ambonya.
Hata hivyo, Dkt Raphael akijibu hoja hizo amesema chanjo hiyo haihusiani na kuongeza nguvu za kiume au kupunguza hivyo mtu anapaswa kuchanjwa ili kujilinda na Uviko-19 na siyo vinginevyo.
“Unapochanja chanjo ya Uviko-19 unakuwa umejiandaa na mapambano kuna baadhi ya watu kwenye mataifa ya nje walipata chanjo kwenye wimbi la pili ila lilipokuja wimbi la tatu chanjo ikawa inawasaidia,” amesema Dkt Raphael.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikitaja takwimu za watu wanaopata maambukizi ya Uviko-19 hivyo wenyeviti hao wasiofie suala la kutangaza idadi ya walioambukizwa.
Amesema suala la vyeti vya kielektroniki litafanyiwa kazi na vyeti hivyo kufikishwa kwa wahusika na kuhusu kujaza fomu na kuandika taarifa huo ni utaratibu wa Wizara ya Afya ili kupata taarifa za waliopata chanjo hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Christopher Chengula amesema amepata chanjo baada ya kupatiwa elimu na maofisa wa afya wa wilaya hiyo.
“Nawahamasisha viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla kushiriki chanjo ya Uviko-19 kwani haina ubaya wataalamu wetu wameshatuhakikishia ni imara hivyo tusipotoshwe na wasio na taaluma ya afya,” amesema Chengula.