Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wakizibua valvu za mgonjwa zilizokuwa zimeziba katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya wiki mbili inayoendelea katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 19 ambao ni watoto na watu wazima wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kifua katika kambi hiyo.
Picha na JKCI
………………….
Na Mwandishi Maalum
Jumla ya wagonjwa 19 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani.
Kambi hiyo ya matibabu ya moyo ya wiki mbili inafanywa kwa watoto na watu wazima wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo JKCI, Peter Kisenge alisema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameruhusiwa kwenda nyumbani.
Alisema hadi sasa wagonjwa watu wazima waliofanyiwa upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua ni sita ambapo watatu walizibuliwa valvu ambazo hazikuwa zinafanya kazi vizuri na watatu walizibwa matundu kwenye moyo.
Aliongeza kwamba watu wazima wawili walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na kubadilishwa valvu zilizokuwa na shida na kuwekewa nyingine za bandia.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Sulende Kubhoja alisema katika kambi hiyo pia wamefanya upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua kwa watoto kumi na moja ambao hali zao zinaendelea vizuri.
Dkt. Kubhoja ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya moyo kwa watoto alisema pamoja na kutoa huduma ya upasuaji katika kambi hiyo pia wanafanya uchunguzi kila siku kwa watoto 20 ambao wanaokutwa na matatizo makubwa wanafanyiwa upasuaji.
Alisema faida ya kambi hiyo ni watoto wanapata huduma katika mazingira rafiki ya nyumbani, madaktari wanapata mafunzo, kubadilishana ujuzi wa kazi na Taasisi kupata vifaa tiba ambavyo ni vya gharama wanavyokuja navyo wageni kwa ajili ya kuvitumia kwa wagonjwa wakati wanafanyiwa upasuaji.
Naye Jenifer Batengi ambaye alifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na sasa ameruhusiwa kutoka Hospitali alisema mwezi wa pili mwaka huu akiwa nyumbani kwake Mbagala alikwenda kuchota maji kwenye ndoo ya ujazo wa lita 20 baada ya kubeba ndoo alikosa pumzi na kuanguka chini.
“Nilipewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na baada ya kufanyiwa vipimo nilikutwa na tatizo katika valvu zangu mbili. Baada ya vipimo nilianza kutumia dawa lakini moyo ulikuwa unaenda mbio na mwili kuchoka”, alisema Jenifer.
Jenifer alimalizia kwa kuwashukuru wataalamu wa afya wa JKCI na madaktari Afrika kwa huduma ya matibabu aliyoyapata na kusema baada ya kufanyiwa upasuaji na kuzibuliwa valvu mbili ambazo zilikuwa na shida anaendelea vizuri kwani anapata pumzi ya kutosha na kutembea vizuri tofauti na ilivyokuwa mwanzo.