Baadhi ya washiriki wakiwa katika Kongamano hili la 34 Chama cha Watalaam wa Maabara Tanzania (MeLSAT) liloanza leo mjini Tabora.
Picha na Tiganya Vincent
NA TIGANYA VINCENT
MKOA wa Tabora umeshapokea zaidi ya bilioni zaidi billion 18 kwa ajili ya kuboresha kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akifungua Kongamano hili la 34 Chama cha Watalaam wa Maabara Tanzania (MeLSAT).
Alisema fedha hizo zimeuwezesha Mkoa wa Tabora kujenga Hospitali mpya 4 katika Halmashauri ya Uyui, Sikonge, Tabora Manispaa na Kaliua, kujenga na kukarabati vituo vya afya 19 na Zahanati 28.
Balozi Dkt. Batilda aliongeza kuwa kupitia fedha za tozo za miamala Mkoa wa Tabora umepokea kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya vinne katika Tarafa zisizokuwa na vituo vya Afya katika Halmashauri za Kaliua, Uyui, Nzega DC na Igunga.
“Napenda kutoa salamu na shukurani zangu za pekee kwa niaba ya wakazi wa Mkoa wa Tabora, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha huduma za afya katika Mkoa wa Tabora” alisema.
Aidha ,Balozi Dkt. Batilda aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo, imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa kimaabara na kutoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu.
Alisisitiza kuwa Serikali imeongeza ujenzi wa maabara mbalimbali na kuziboresha si zile Hospitali za mikoa pekee, bali maabara katika Hospitali za Wilaya na sasa katika Vituo vya afya.
Balozi Dkt. Batilda alisema ujenzi huu unakwenda sambamba na ufungaji wa mashine bora za kufanya vipimo mbalimbali.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watalaam wa maabara, kuhakikisha wanavitumia kwa usahihi na kuvitunza na kufanyakazi kwa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma yao ili waweze kutoa majibu sahihi kwa wagonjwa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa alisema Watalaam wa Maabara ni kiungo muhimu katika ya Daktari na Mgonjwa.
Alisema matokeo ya vipimo yanayotolewa na Watalaam wa Maabara ndio yanamsaidie Daktari kubaini tatizo linalomsumbua mgonjwa na kumuandikia dawa.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa aliwataka watalaamu wa maabara kuendelea na mapambano dhidi ya milipuko ikiwemo janga la UVIKO – 19 kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 inayoendelea kutolewa nchi nzima.
Alisema lengo la Chanjo ambazo hutolewa bila malipo inalenga kumlinda Mtanzania ambaye anategemea kwenye ujenzi wa uchumi.
Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu aliwataka Wataalamu wa Maabara hapa nchini kuwekeza kupitia fursa ya Tabora kupakana na mikoa mingi kuwekeza katika vifaa vya uchunguzi wa magonjwa ya binadamu.