Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akishuka katika helkopta wakati yeye na timu yake ya Mawaziri wa Kisekta walipowasili katika kijiji cha Mwombose wilayani Chemba kuzungumza na wananchi kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa vijiji vya Bubutole na Mwombose wilayani Chemba mkoani Dodoma wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi
Sehemu ya wananchi wa vijiji vya wa vijiji vya Bubutole na Mwombose wilayani Chemba mkoani Dodoma wakifuatia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mawaziri wa kisekta wakati wa ziara ya kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi
Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Mery Masanja akizungumza na wananchi wa vijiji vya Bubutole na Mwombose wilayani Chemba mkoani Dodoma wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi
Waziri wa Maji Jumaa Awesu akizungumza na wananchi wa vijiji vya Bubutole na Mwombose wilayani Chemba mkoani Dodoma wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi
……………………………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM CHEMBA
Serikali imevibakisha vijiji 40 kati ya 42 ambavyo wananchi wake walikuwa wakiishi na kuendesha shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba katika mkoa wa Dodoma.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wananchi wa vijiji hivyo kuendelea na shughuli zao baaada ya kuwepo mgogoro wa matumizi ya ardhi uliosababisha kuundwa kwa Timu ya wataalamu iliyoongozwa na mawaziri nane kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Bubutole na Mwombose vilivyo katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma tarehe 5 Oktoba 2021 katika ziara ya Mawaziri nane kutoa mrejesho wa ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema uamuzi huo unafuatia serikali kuamua kufuta mapori 12 yenye ukubwa wa ekari 707, 659 na ekari 46,755 za misitu 12 kwa ajili ya kuwamegea wananchi sehemu ya maeneo hayo ili kuendesha shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo na ufugaji.
“Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ni kuondoa shaka na taharuki kwa wananchi wanaoishi kwenye vijiji husika” alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alisema, tayari GN za Misitu na Mapori ya akiba vilivyokuwemo vijiji hivyo imefutwa na sasa taasisi zenye dhamana na maeneo ya hifadhi zinatakiwa kulinda na kuweka alama za mipaka kwenye maeneo yaliyobaki kwa lengo la kuepusha kuvamiwa na wananchi.
Lukuvi ambaye ni kiongozi wa kamati ya Mawaziri nane alisema, vijiji viwili kati ya 42 katika mkoa huo wa Dodoma itabidi viondolewe kupisha ujenzi wa bwawa la maji la Farkwa katika wilaya ya Chemba na vijiji hivyo ni Bubutole na Mwombose vilivyopo katika wilaya ya Chemba.
‘’Serikali tayari imelipa fidia kwa wananchi katika vijiji hivi na wale ambao fidia haikwenda vizuri serikali ipo na kila mtu lazima alipwe kulingana na mali zake na na Rais wetu Mhe.Samia Suluhu ameshatoa fedha kwa ajili ya huduma za shule, zahanati pamoja na maji pale mtakapokwenda’’. Alisema Lukuvi.
Tayari wakazi 2,829 sawa na asilimia 99 kati ya 2,868 katika vijiji hivyo viwili wameshalipwa fidia.
Bwawa litakalojengwa litakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 68 na mm za ujazo milioni 470 na litanufaisha wakazi wa jiji la Dodoma, Chemba, Bahi na Chamwino pamoja na vijiji vyote vitakavyopitiwa na bomba hilo.
Hata hivyo, Lukuvi alisema, pamoja na serikali kubakisha vijiji 40 katika mkoa wa Dodoma baadhi ya vitongoji navyo vitafanyiwa tathimini upya ili kuondoa kasoro zilizojitokeza awali na kusisitiza kuwa tathmini hiyo itakuwa shirikishi kwa viongozi, wataalamu na wananchi wa vitongoji husika.
“Vijiji vyote 40 katika mkoa huu wa Dodoma vitabaki ila ndani ya vijiji 20 kuna vitongoji tutavifanyia tathmini upya na suala hili litakuwa shirikishi” alisema Lukuvi.
Mawaziri nane kutoka wizara za kisekta wameanza ziara katika katika vitongoji vilivyopo vijiji vya Handa na kuzungumza na wananchi wa kitongoji cha Mbugani katika hifadhi ya pori la Swagaswaga na kuendelea na vijiji vya Bubutole na Mwombose kwa lengo la kutoa mrejesho ikiwa ni utekelezaji agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa 7 Agosti 2021 kutaka kutekelezwa kwa ufumbuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 bila kuleta taharuki kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa ambapo mrejesho huo umeanza katika vijiji 920.