Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi akihutubia Machifu na Viongozi wa Kimila katika Kikao kilichoandaliwa na Wizara hiyo kujadili na kuchukua maoni ya Viongozi hao katika kuboresha Sera ya Taifa ya Utamaduni, Kikao kilichofanyika Oktoba 5, 2021 Jijini Dodoma ambapo Dkt. Abbasi amekuwa Mgeni Rasmi katika Kikao hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi akizawadiwa fimbo kutoka kwa Kiongozi wa Kimila wa Jamii ya Wamasai baada ya kumalizika kwa Kikao kilichoandaliwa na Wizara hiyo kujadili na kuchukua maoni ya Viongozi hao katika kuboresha Sera ya Taifa ya Utamaduni, Kikao kilichofanyika Oktoba 5, 2021 Jijini Dodoma ambapo Dkt. Abbasi amekuwa Mgeni Rasmi katika Kikao hicho.
Baadhi ya Machifu na Viongozi wa Kimila walioshiriki katika Kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kujadili na kuchukua maoni ya Viongozi hao katika kuboresha Sera ya Taifa ya Utamaduni, Kikao kilichofanyika Oktoba 5, 2021 Jijini Dodoma ambapo Dkt. Abbasi amekuwa Mgeni Rasmi katika Kikao hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi (aliyekaa katikati) akiongoza mjadala wa kukusanya maoni kutoka kwa Machifu na Viongozi wa Kimila ambao wamekutana leo Oktoba 5, 2021 kujadili na kuchukua maoni ya Viongozi hao katika kuboresha Sera ya Taifa ya Utamaduni. Viongozi wengine kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Emmanuel Temu na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Msagata Fundikila.
**********************************
Na John Mapepele, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amewataka Machifu na Viongozi wa Kimila kushirikiana na Serikali kuhamasisha michezo ya jadi ili michezo hiyo iwe na tija kwenye mashindano ya kombe la taifa yanayoanza kurindima hivi karibuni.
Dkt. Abbasi amesema hayo leo wakati akitoa maazimio ya kikao cha pamoja baina ya Wizara, Machifu na Viongozi wa Kimila kuhusu utoaji wa maoni ya kuhuisha Sera ya Utamaduni leo Oktoba 05, 2021 katika ukumbi wa African Dreams jijini Dodoma.
“Serikali imeamua kufufua na kuboresha mashindano ya Kombe la Taifa ambapo tumeijumuisha michezo ya jadi kutokana na umuhimu wake hivyo natoa wito kwenu kuhamasisha michezo hii ambayo inaanzia kwenye ngazi za vijiji ili iweze kuwa na athari chanya kwenye mashindano ya Taifa ya mwaka huu”. Ameongeza Dkt. Abbasi
Amefafanua kuwa miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni Machifu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda amani na ustawi wa jamii ya wananchi wa Tanzania.
Ametoa siku saba za kuendelea kutoka maoni ya kuboresha Sera hiyo ambapo amesema baada ya hapo zoezi hilo litaendelea katika ngazi za juu.
Pia ametoa siku 30 kwa Machifu kuwasilisha maeneo ya kimila na kiutamaduni ili Serikali iweze kuyatambua na kuyafanyia kazi.
Makamu Mwenyekiti wa (UMT) ambaye pia ni Chifu wa Unyanyembe Tabora Chifu Msagata Fundikila ameipongeza Serikali kwa kuwashirikisha Machifu katika kikao hicho.
Amesema kikao hiki kimekuja katika wakati mwafaka kwa kuwa utamaduni wa taifa umekuwa ukiharibiwa na utandawazi.
Makamu Katibu Mkuu wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) nchini Amani Lukumai amesema kuna haja kwa Serikali kuendelea na utoaji wa elimu wa umuhimu na uzuri wa utamaduni na mila.
Aidha, ameongeza kuwa ni muhimu kwa Serikali kufanya utafiti wa namna gani nchi mbalimbali duniani kama China wamefanikiwa kuulinda utamaduni wao.
Kikao hiki kinafuatia maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Tamasha la Utamaduni lilioandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania (MUT) Septemba 8, 2021 jijini Mwanza.
Rais Samia aliitaka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo iwashirikishe Machifu katika kuhuisha Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997.
Zaidi ya Machifu na Viongozi wa Kimila 105 kutoka mikoa yote nchini wamehudhuria.