Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mara baada ya kuwasili katika ziara yake Mkoani hapo kukagua shughuli mbalimbali za Maendeleo.
Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya watoto Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer akimuonesha Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis maeneo mbalimbali ya Mahakama hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa zawadi kwa ajili ya mahabusu ya watoto Mbeya alipofanya ziara ya kukagua uendeshaji wa mahabusu hiyo iliyopo Jijini Mbeya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akipata maelezo ya baadhi ya wanafunzi waliohitimu Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole na kuweza kumudu maisha yao kwa kutumia ujuzi walioupata kubuni na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikata utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi wa madarasa mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 200 kila moja katika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Uyole Mbeya. Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho Rajab Sadick, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Rashid Chuachua.
Watumishi na baadhi ya wanachuo cha Uyole wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (hayupo pichani) akizungumza nao alipotembelea chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiangalia zawadi aliyopewa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole alipotembelea chuo hicho katika ziara yake Mkoani Mbeya.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
……………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Wananchi wa Mkoa wa Mbeya na Mikoa jirani wametakiwa kukitumia vizuri chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole kilichopo Jijini Mbeya ili kuhakikisha kinawasaidia kufikia malengo na Maendeleo endelevu kwa manufaa yao na Taifa kwa Ujumla.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika Chuo hicho alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa madarasa mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400.
Mhe. Mwanaidi amesema Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ni msingi wa vijana kuweza kushirikiana na jamii zao kuibua changamoto na kuzifanyia kazi kutokana na ujuzi wanaopata.
“Nimejionea wenyewe wanafunzi wa Chuo hiki vitu wanavyobuni miradi kwa ajili ya Maendeleo ya Jamii na Taifa katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kujenga vyoo zaidi ya 200 ili kuwaepusha wananchi na magonjwa mbalimbali ya mlipuko” amesema Mhe. Mwanaidi.
Mhe . Mwanaidi ameipongeza Idara ya Maendeleo ya Jamii mkoani Mbeya kwa kushirikiana vyema Chuo hicho na vyuo vingine kwa kuandaa miongozo na kusisitiza utoaji wa mafunzo unaolenga kuweza kujiajiri na kuajiri wengine.
“Hili inadhihirisha kuwa kwa uwepo wa programu za uanagenzi inayofanywa na wanachuo kujikita katika kuwajengea umahiri katika fani wanazochagua ambazo zitawasaidia kwenye maisha yao” amesema Mhe. Mwanaidi.
Aidha, ameutaka uongozi wa Chuo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa madarasa hayo yatakayojengwa kwa gharama ya sh. milioni 124 ili kuongeza udahili wa wanafunzi na kupunguza changamoto ya madarasa chuoni hapo.
Mhe. Mwanaidi amesema madarasa hayo yatawezesha wanafunzi wengi kujiunga na Chuo hicho kuwa faida ya maisha yao na Jamii na kwamba Wizara itaendelea kukiendeleza kwa kutatua changamoto ikiwemo kuongeza mabweni na kuongeza watumishi kadri fedha itakavyopatikana.
Akizungumza na watumishi wa Chuo hicho Mhe. Mwanaidi amesema mbali na kuchangia kuwainua watoto kwa kutoa elimu, Chuo hicho kina umuhimu mkubwa katika kuchangia Maendeleo ya Mkoa.
Akiwa chuoni hapo, Mhe. Mwanaidi ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea kujikinga na UVIKO19 hasa kwa kujitokeza kuchanja ili kujikinga na madhara ya ugonjwa huo.
Awali, Mkuu wa Chuo hicho Rajab Sadick akiwasilisha taarifa alisema wameendelea kupanua wigo Kwa kuongeza udahili wa wanafunzi Kwa asilimia 62.3 tangu mwaka 2018 hadi 2021 ambapo jumla ya wanachuo 1791 wamedahiliwa.
Rajab ameongeza kuwa, wamedhamiria kutatua matatizo ya vijana kupanga mitaani kwa kujenga bweni litakalochukua wanafunzi 600 kwa sh. bil 2.8 na kuiomba Wizara iendelee kusaidia upatikanaji wa fedha.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo, Mhe. Rashid Chuachua amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika Mkoa wa Mbeya ambapo wamepiga hatua kubwa ya Maendeleo katika sekta nyingi.
Akizungumza Kwa niaba ya wananchi wa kata ya Uyole kilipo Chuo hicho, Diwani wa kata hiyo Mhe. Daniel Njango amesema Chuo hicho kimeonesha Maendeleo ya kweli ndani na nje ya Kata ya Uyole ambao watu wa kwanza kunufaika wamekuwa ni wananchi wa vijiji vya ndani na nje ya kata ya Uyole.
“Chuo kina ushirikiano mkubwa na Jamii ikiwemo kuwajengea choo bora na ujenzi wa sekondari, tunahitaji elimu yao kwenye mchango wa Maendeleo ya Jamii yetu” amesema Diwani hiyo.
Naibu Waziri Mwanaidi anaendelea na ziara yake Mkoani Mbeya kukagua shughuli mbalimbali za Maendeleo ya Jamii na kuamsha Ari ya wananchi kujiletea Maendeleo ambapo katika Jiji la Mbeya ametembelea Mahakama ya watoto na Mahabusu ya watoto na kuzungumza na watumishi.