NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewagiza Mradi wa Kijana Jitambue kupelekwa katika shule nyingi kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike kukabiliana na vikwazo vinavyokatisha ndoto zao za kupata elimu.
Alisema mradi huo unatakiwa kupanua wigo kwa kuwaweza watoto wa kike kutimiza maono yao kwa kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa Mabweni kwa ajili yao ili kuepuka hatari ya kupata ujauzito.
Balozi Dkt. Batilda alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mradi wa kuboresha elimu ndani na nje ya mfumo rasmi wa shule ujulikanao kama Kijana jitambue unaotekezwa kwenye Halmashauri za Wilaya Nane za Mikoa ya Tabora na Shinyanga.
Alisema changamoto inayokwamisha ndoto za baadhi ya watoto kike katika Mikoa ya Tabora na Shinyanga ni mimba za utotoni ambazo wanazipata kutokana na kusafiri umbali mrefu kutoka kwao hadi shuleni na kupita katika maeneo mengine ambayo ni hatarishi.
Balozi Dkt. Batilda alisema msaada mkubwa kwao ni kuwajengea Mabweni ili waweze kuishi katika maeneo ya shule na kuwa na mazingira mazuri ya kusoma na kujifunza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati aliwashukuru Shirika la Care International kwa kuweza kushirikiana na Serikali katika utoaji wa mafunzo ya stadi za ujasiriamali, ufundi wa awali kama vile useremala, uashi, ushonaji na uchomeleaji kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa shule.
Alisema hiyo ni fursa adhimu kwa vijana hao ambao itasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira ambapo baadhi yao wasingepata mafunzo hayo wangejihusisha na vitendo vya wizi, uporaji wa mali za watu , uvutaji bangi na mambo mengine yasiyofaa katika jamii.
Dkt. Sengati alisema maendeleo yanapswa kushirikisha wadau wote wakiwemo Washirika wa maendeleo, wananchi na Serikali.
Mkurugenzi Mkazi wa Programu ya Shirika la Care International Haika Mtui alisema kuwa mradi wa kijana Jitambue unatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya nane kutoka Tabora na Shinyanga.
Alisema mradi huo ambao umelenga kuongeza usawa katika upatikanaji wa elimu kwa vijana hasa wasichana ambao wanaishi katika mazingira magumu umeanza mwaka huu utamalizika mwaka 2023 na utagharimu kiasi cha bilioni 2.3.
Haika alisema mradi huo utawajengea uwezo kwa vijana na hasa watoto wa kike kutimiza malengo ya kujisimia katika maisha yao na kuwa na taarifa sahihi za afya ya uzazi.