Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo October 1,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya utekelezaji wa kupambana na rushwa kwa robo ya Julai hadi Septemba,2021
…………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo,amesema kuwa wameanza kufuatilia utekelezaji wa Miradi miwili yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni 10 ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana.
Hayo ameyasema leo October 1,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya utekelezaji wa kupambana na rushwa kwa robo ya Julai hadi Septemba,2021
Bw. Kibwengo amesema ufuatiliaji huo unafanywa kwa kushirikiana na Wakal wa Barabara za vijijini (TARURA) na Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Dodoma.
“Agost mwaka huu TARURA mkoa wa Dodoma ilisaini mikataba 43 na wakandarasi mbalimbali kwa kazi ya ujenzi wa barabara katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma zenye thamani ya jumla ya sh.10.213 inayotekelezwa awamu ya kwanza kwa mwaka 2021/2022”amesema
Ameeleza kuwa RUWASA iligawanya mabomba yenye urefu wa mita 35,232 katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Mpango wa Malipo kwa Matokeo awamu ya nne ambapo gharama za ulazaji wa mabomba hayo zinakadiriwa kuwa sh.95.198 .
Hata hivyo Kibwengo amewaomba wananchi katika maeneo yanayotekelezwa miradi hiyo kuwa makini kuifutilia kwani ushirikiano wao ni silaha muhimu ya kufikia lengo la miradi hiyo.
”Nawataka wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kutimiza wajibu wao kwa weledi na uaminifu kwa kufuata sheria na taratibu”amesema’
Pia amefafanua kuwa taasisi hiyo imekagua miradi mingine 17 kwenye sekta za Elimu ,afya na kilimo kwa lengo la kuhakikisha fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi hiyo zinatumika kwa ufanisi na uaminifu.
Amesema kuwa katika kufuatilia miradi hiyo kumewezesha kuokoa na kudhibiti fedha na vifaa vyenye jumla ya sh.47.827 ambapo kati yake ni vifaa vyenye thamani ya shilingi 41.950 vilivyochepushwa kutoka kwenye mradi wa ujenzi wa hospitali moja.
Aidha Kibwengo amesema katika robo ya Oktoba hadi Disemba mwaka huu imeweka msisitizo katika kuwashirikisha vijana kupitia ushirika wa utatu wa TAKUKURU ,Chama CH Skauti Tanzania na Idara ya Walimu .
“Vijana wa skauti wataelimishwa kuhusu mbinu na umuhimu wa kishiriki katika kuzuia rushwa ili nao wafikishe elimu hiyo kwa vijana wenzao,nyumbani na kwenye jamii kwa ujumla.” Amesema Kibwengo
Aidha amewaomba wananchi wa Mkoa wa Dodoma kutokuwa watazamaji katika mapambano dhidi ya rushwa bali kushiriki kivitendo kukemea na kuwa mfano mwema wa tabia njema kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.