Ofisa wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Boniface Mushi (wapili kushoto) akishuhudia maji yakitoka shule ya msingi Endiamtu mji mdogo wa Mirerani, baada ya huduma hiyo kurejea shuleni hapo.
************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI wa shule ya msingi Endiamtu, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, wameishukuru Serikali kwa kurejesha maji ya bomba yaliyokatwa shuleni hapo.
Hata hivyo, wamewapongeza waandishi wa habari walioibua na kuandika kwenye vyombo vya habari changamoto ya ukosefu wa maji na serikali kuchukua hatua.
Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo Juma Said, amesema walikuwa wanatoa maji na madumu nyumbani na kupeleka shuleni ila hivi sasa kuna maji ya bomba.
“Tunaishukuru serikali kwa kuturudishia maji na unawapongeza waandishi na vyombo vya habari vilivyoandika kero yetu ya maji hadi tukarudishiwa maji,” amesema.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Chimbason Zacharia, ameishukuru Serikali kwa kufanikisha urejeshaji na upatikanaji wa maji hayo.
“Halikuwa jambo zuri kwa watoto wetu kutoka nyumbani kwenda shuleni na kubeba madumu ya maji ila tunaipongeza Serikali kwa kufanikisha hili,” amesema Luka.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Endiamtu, Anthony Jacob Mavili amepongeza hatua hiyo kwa Serikali kufanyia kazi changamoto ya maji.
“Ziara ya kamati ya siasa ya CCM Kata ya Endiamtu imekuja na mafanikio, sisi kazi yetu ni kuisimamia Serikali ili itekeleze ilani na ndivyo tulivyofanya,” amesema.
Hata hivyo, meneja wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martin, ameutaka uongozi wa shule hiyo kutunza miundombinu ya maji hayo.
Mhandisi Martin amesema pia uongozi wa shule hiyo unapaswa kutimiza wajibu wao kwa kulipa ankara ya maji wanayotumia kwa wakati.