Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane itakayopitiwa na bomba la mafuta kuwasili katika eneo la Chongoleani Tanga, tarehe 29 Septemba, 2021 mahali ambapo bandari itajengwa. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Adam Malima.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Adam Malima, akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane itakayopitiwa na bomba la mafuta kuwasili katika eneo la Chongoleani Tanga, tarehe 29 Septemba, 2021 mahali ambapo bandari itajengwa. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akiangalia jiwe la msingi lililowekwa eneo la Chongoleani Tanga mahali ambapo bandari itajengwa wakati Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane itakayopitiwa na bomba la mafuta walipotembelea eneo hilo tarehe 29 Septemba, 2021
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge, akizungumza na waandishi wa Habari wakati Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane itakayopitiwa na bomba la mafuta walipotembelea eneo hilo la Chongoleani Tanga tarehe 29 Septemba, 2021 mahali ambapo bandari itajengwa. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato.
…………………………………………………………………
Na Dorina Makaya & Janeth Mesomapya
Naibu Waziri wa Nishati Wakili Stephen Byabato ameongoza timu ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane (8) ambapo utapita mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) na baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi za umma kufanya ziara katika eneo utakapoishia mradi huo Chongoleani, jijini Tanga.
Katika ziara hiyo, Wakili Byabato ameeleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha manufaa yatakayotokana na mradi huo yanawanufaisha kwanza wakazi wa maeneo ambayo bomba hilo litapita.
“Tunatambua kuwa
mradi huu utalinufaisha taifa kiuchumi lakini tunahitaji uanze ngazi ya chini kabisa ya wananchi ambao maeneo yao yatapitiwa na bomba hili, na hii ndio maana halisi ya ushirikishwaji wa wazawa katika miradi ya maendeleo,” aliongeza.
Ameongeza kuwa kwa kutekeleza hilo, Waziri wa Nishati, Mh. January Yusuf Makamba amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Nishati kushirikiana na sekretarieti za mikoa hiyo minane kutengeneza maelezo mahususi ya mikoa hiyo yatakayofanikisha unufaikaji wa fursa zitokanazo na utekelezaji wa mradi huo.
Naibu Waziri Byabato amehitimisha semina hiyo maalumu ya siku tatu iliyoandaliwa kwa lengo la kutoa uelewa wa mradi na fursa zitakazotokana na utekelezaji wake kwa viongozi hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mh. Adam Malima amesema kwamba mradi huu utavutia fursa nyingi zaidi za uwekezaji nchini kupitia bandari ya Tanga, hivyo ni vyema wananchi hususani wa mkoa wa Tanga wakajiandaa ili kuchangamkia fursa hizo.