Waziri Januari Makamba akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Donald Concar. Kushoto kwa Balozi ni Mshauri wa Balozi kuhusu Maendeleo ya Sekta Binafsi, Tom Ratsakatika.
Balozi wa Uingereza nchini, Donald Concar akizungumza na Waziri wa Nishati, January Makamba.
Waziri wa Nishati, January Makamba akiwa na mgeni wake, Balozi wa Uingereza nchini, Donald Concar alipomtembelea ofisini kwake hivi karibuni kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Nishati Dar es Salaam
Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Donald Concar (hayupo pichani) alipomtembelea kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Nishati, Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali.
………………………………………………………………
*Ataka nishati jadidifu itumiwe ipasavyo
*Asisitiza sera ya umeme wa tungamotaka
Na Dorina Makaya & Janeth Mesomapya
NISHATI ya umeme ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa lolote lile, na hivyo ili kujihakikishia maendeleo hayo, ni vema kujizatiti kwa kuwa na uhakika wa nishati hiyo.
Waziri wa Nishati, January Makamba analijua hilo na ndiyo sababu katika dhamana aliyonayo hivi sasa, ameamua kwa dhati kabisa kuhakikisha umeme haukatikikatiki na hivyo kuwezesha uhakika wa uzalishaji mali.
Amebainisha hayo baada ya kukutana na ujumbe wa Uingereza ulioongozwa na Balozi wa nchi hiyo, David Concar ukitaka kujua kuhusu utekelezaji na uwekezaji katika nishati jadidifu na hatua iliyofikiwa.
Ni kawaida kwamba kila anapoingia waziri mpya katika Wizara, mabalozi wanaowakilisha nchi zao huwa na shauku ya kutaka kujua vipaumbele vya Waziri katika sekta husika.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Waziri Makamba katika sekta ya nishati ikiwamo gesi.
Akizungumza na Balozi Concar, Waziri Makamba alisema, katika upande wa nishati Wizara yake ilikuwa awali imejikita kwenye umeme wa kawaida badala ya kujikita kwenye nishati ya mafuta, gesi na umeme.
Hivyo Waziri Makamba akasema, ataweka msisitizo sana kwenye nishati jadidifu ambayo ni ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya jua na upepo.
Lakini pamoja na kazi zinazoendelea sasa hivi, alisema ataangalia kikubwa kingine, kwamba atalenga kupunguza matumizi ya mkaa ili kuachana na matumizi ya mkaa hususan katika Jiji la Dar es Salaam.
Hiyo ni kwa sababu Dar es Salaam ndilo jiji nchini, linaloongoza kwa kupatiwa umeme, lakini pia linaongoza kwa matumizi makubwa ya mkaa.
Hivyo Waziri Makamba akawaelekeza wataalamu kuibua mradi wa namna ya kuachana na matumizi ya mkaa Dar es Salaam na kwa nchi nzima kiujumla, ili kulinda mazingira.
Kwa upande wa ujumbe wa Uingereza walikuwa na masuala ya uwekezaji katika miradi ya uzalishaji nishati ya umeme kutokana na nguvu ya jua na upepo, ambapo ulionesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo.
Hivyo, ubalozi wa Uingereza ukataka kujua Serikali ya Tanzania imejiandaaje na kama kuna fursa za kuwekeza ambapo Waziri wa Nishati, Makamba aliuambia kwamba fursa hizo zipo.
Aidha, ubalozi huo ukataka kujua, kuhusu Mpango Kabambe wa Nishati Tanzania unasemaje, ambapo Wizara ya Nishati imepanga ifikapo mwaka 2025 kuwe na megawati zisizopungua 700.
“Kwa sababu tunataka tuwe na megawati 350 kutokana na jua na 350 za upepo lakini kwa kuanzia, Wizara ya Nishati ilipanga kuanza na megawati 350 hadi ilipofika mwaka jana, za jua zikiwa 150 na 200 za upepo,” aliosema Waziri Makamba.
Aliongeza kuwa “kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 tunatakiwa tufikishe megawati 700. Jua likizalisha megawati 350 huku 350 zikitokana na upepo na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa,” alisema Waziri wa Nishati akisisitiza kuwa huo ndio utakuwa mpango wake.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Makamba aliwataka wataalamu wa Wizara yake kuandaa sera kuhusu tungamotaka (Biomas), kwa sababu imeonekana nchini asilimia 80 ya nishati inatokana na taka.
Kwa sasa Wizara ya Nishati haina sera ya tungamotaka , hivyo Waziri Makamba aliwaelekeza wataalamu kuiandaa ikionesha matumizi ya tungamotaka, na kwa maana hiyo isaidie kupunguza matumizi ya mkaa na kulinda mazingira.
Ujumbe huo wa Uingereza ulijielekeza pia katika suala la kuzalisha umeme kwa kutumia wazalishaji wadogo, ukitaka kujua Serikali imefikia hatua gani katika majadiliano kuhusu gharama za uwekezaji katika kuzalisha umeme kutokana na vyanzo vidogo.
Lakini huko nyuma, Serikali ilishatoa maelekezo kuhusu viwango vya bei kwa wazalishaji hao wa umeme, kutumia vyanzo vidogo, kutokana na kuwa na viwango tofauti vya bei, ambapo kila mzalishaji mdogo alitoza bei yake katika maeneo mbalimbali.
Mwaka jana Serikali ilitoa maelekezo kwa wazalishaji wadogo wote, kwamba watoze viwango vya bei sawa na vya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ubalozi wa Uingereza ulilenga kuendelea kusaidia wazalishaji umeme wadogo, ili waendelee kuzalisha nishati hiyo na kuchangia kwenye uzalishaji wa nchi lakini wanashindwa kufanya hivyo, kwa sababu viwango vinavyotozwa vinashindwa kurudisha faida.
Kutokana na nia hiyo njema ya Uingereza, Waziri Makamba akaahidi kulipitia suala hilo vema na kulitolea uamuzi.
Kwa hatua hiyo, Uingereza ilionesha nia ya kuwekeza katika miradi ya nishati jadidifu, ambayo ni ya kuzalisha umeme wa jua na upepo na kuwa tayari kusaidia Tanzania katika eneo hilo.
Kupitia Balozi Concar, Uingereza ilisema inasubiri kujua kwamba Serikali ya Tanzania na hasa uongozi mpya wa Wizara ya Nishati umejiandaaje katika eneo hilo.
Waziri Makamba alisema kuanzia sasa ataelekeza nguvu katika nishati jadidifu, kwa sababu anaona huku kwingine hatua imeshapigwa sana na hivyo hapana sababu kila mara kuzungumzia gesi na maji.
Hivyo, ni wakati sasa kuzungumzia upepo na jua.
Aliahidi kuja na mikakati ya kuhakikisha Tanzania inazalisha umeme wa jua na upepo.
Wizara ya Mishati ina Sera ya Nishati yaTaifa ya mwaka 2015 lakini imejumuisha nishati zote pamoja; yaani mafuta, gesi, tungamotaka na umeme wa kawaida.
Kwa hiyo Waziri Makamba anataka kwa kuwa tungamotaka mchango wake ni mkubwa kwa zaidi ya asilimia 80, ni bora kuwa na sera ya tungamotaka, ili kusimamia vizuri chanzo hicho cha umeme.
Lakini lingine ni kutaka matumizi ya LPG yafike sehemu zote. Kwani REA ni Rural Energy Agency kwa maana ya Wakala wa Nishati Vijijini na si Rural Electrification Agency yaani Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini.
Hivyo kama REA ni wakala wa nishati, basi ipo sababu ya kuhakikisha nishati zote zinasambazwa katika vijiji nchini si tu umeme peke yake, bali pia nishati ya umeme wa gesi na wa vyanzo vingine.
Hivyo, kwa sasa hivyo ndivyo vipaumbele vya Waziri Makamba.