Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba akifungua warsha ya kukuza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango kazi wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu (2020 -2025),iliyofanyika leo September 28,2021 jijini Dodoma.
Waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali wakiwa katika ziara ya mafunzo kwenye machimbo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu ya Chikowa jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya warsha ya kukuza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango kazi wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu (2020 -2025),iliyofanyika September 28, 2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua warsha ya kukuza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango kazi wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu (2020 -2025),iliyofanyika leo September 28,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba amesema nyenzo kubwa ya kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ni kutoa elimu kwa kundi hilo.
Dkt. Komba amesema hayo leo Septemba 28, 2021 wakati akifungua warsha ya kukuza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango kazi wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu (2020 -2025), iliyofanyika jijini Dodoma.
Alisema Tanzania ilitekeleza mradi wa kuandaa Mpango kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki ambao ni wa miaka mitano (2020 – 2025) kwa lengo la kupunguza na pale inapowezekana kuondosha matumizi ya kemikali hiyo katika shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kulinda afya ya binadamu na mazingira.
Aidha, Dkt. Komba alisema pamoja na kuwa na lengo kuu la kupunguza matumizi ya Zebaki vilevile unalenga kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala ili kupunguza changamoto za afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.
“Uchimbaji huu mdogo wa dhahabu nchini hutumia kemikali ya Zebaki katika kuchenjua dhahabu. Pamoja na faida kubwa inayopatikana kutokana na sekta hii, shughuli hizi zimekuwa na changamoto kubwa katika afya ya binadamu na mazingira ikiwa ni pamoja na umwagaji maji yenye sumu kwenye mazingira, uchafuzi wa hewa unaotokana na uchomaji holela wa dhahabu, uchenjuaji wa dhahabu usiotumia vifaa kinga, ukataji wa miti kwa ajili ya kupata magogo ya kujengea mashimo,” alisema Dkt. Komba.
Mkurugenzi huyo alisema tafiti mbalimbali zimeendelea kufanyika na kubainisha kuwa Zebaki ni chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira duniani ambapo huchangia takriban asilimia 38 ya uchafuzi wa mazingira na hali inaambatana na athari katika afya ya binadamu.
Aidha, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Zebaki inatajwa kuwa ni miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya ya binadamu hivyo kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya kimataifa ilipitisha Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki mwaka 2013 wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira unotokana na Zebaki.
Hivyo, Mpango Kazi huo umeainisha pamoja na mambo mengine Hali ya Sekta ya Wachimbaji Wadogo nchini ilivyo; Malengo na Shabaha Muhimu ya Mpango–Kazi; Mikakati ya Utekelezaji ikihusisha Gharama na Utaratibu wa Utekelezaji; na Uratibu wa Tathmini na Ufuatiliaji.