Joseph Lyimo
Imeelezwa kuwa mtu akipata maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 viungo mbalimbali vya mwili vinapata madhara ikiwemo kupungua kwa nguvu za kiume, kuathirika mifupa na mimba kutoka.
Pia maambukizi ya Uviko-19 husababisha binadamu kupata kiharusi, mapafu hayawezi kurejea kwenye hali yake ya kawaida na tatizo la figo.
Kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Babati Mkoani Manyara Dkt Emmanuel Mkonyi ameyasema hayo wakati akielezea madhara ya Uviko-19 kwenye mwili wa binadamu.
Dkt Mkonyi amesema tafiti mbalimbali ndizo zilizobainisha matatizo hayo kwenye mwili wa binadamu hivyo watu wapate chanjo ya Uviko-19.
Amesema yeye binafsi ameshawahi kupata ugonjwa wa Uviko-19 na amepona ila baada ya kupata chanjo hajaugua tena ugonjwa huo.
Amesema hata alipochanja hakupata tatizo lolote kama baadhi ya watu wanavyosema kuwa unapatwa na kichefuchefu au kuumwa kichwa.
“Kwa hiyo baadhi ya watu wanaopotosha chanjo waache kabisa, kwani chanjo ya Uviko-19 ni bora kabisa hivyo wananchi wachanje bila tatizo lolote,” amesema Dkt Mkonyi.
Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange amesema upatikanaji wa chanjo hivi sasa umeboreshwa katika maeneo mbalimbali ya eneo hilo.
Twange amesema wananchi wote wanapaswa kutambua huduma ya chanjo ya Uviko-19 imeboreshwa na inapatikana vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Amesema pia huduma ya chanjo itatolewa kwenye vituo vya mabasi, sokoni, mashuleni na kwenye taasisi mbalimbali kulingana na uhitaji.
“Ewe mwananchi jitokeze kupata chanjo kwa ajili ya afya yako, chanjo ni salama na ndiyo njia pekee ya kupambana na ugonjwa wa Uviko-19,” amesema Twange.
Mkazi wa mtaa wa Nakwa, Albert Bhukhay amesema chanjo ya Uviko-19 ni muhimu kwa wananchi kwani hata yeye amepatiwa chanjo.
“Serikali imetimiza wajibu wake kwa kutuletea chanjo na sisi tutimize wajibu wetu kwa kuchanja chanjo ya Uviko-19,” amesema.