……………………………………………………………….
Na Damian Kunambi, Njombe
Wakazi wa kata ya Ibumi iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kuwaboreshea mitandao ya simu ili waweze kufanya mawasiliano kwa urahisi kwani kwa sasa wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa moja ili kupata mtandao.
Ombi hilo wamelitoa baada ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasili katika kata hiyo ambapo wananchi hao wamedai pamoja na umbali huo wanaotembea lakini pia wanakosa uhuru wa kuongea kwakuwa hukutana watu wengi mahala pamoja.
Suzana Komba ni miongoni mwa wananchi hao amesema tatizo hilo linawapa tabu sana kwani wanapopata dharula wanashindwa kutoa taarifa hata kwa majirani kitu ambacho ni hatari kwao.
Ameongeza kuwa eneo linalopatikana mtandao wamekuwa wakijaa watu wengi kiasi kwaba kama una mazungumzo ambayo ni faragha inakuwa ni ngumu kuzungumza.
Naye Filbert Kayombo amesema kwa upande wao hawaoni thamani ya kumiliki simu wakati hazina mitandao kwakua muda mwingine wanakaa muda mrefu bila kufanya mawasiliano na ndugu zao kutokana na kushindwa kutembea umbali huo.
“Huu umbali unatutesa sana kiasi kwamba inafika wakati hatuwasiliani na ndugu mara kwa mara na hata thamani ya simu inakuwa haipo maana tunaishia kutumia simu zetu kwa kusikiliza mziki na kuangali video badala ya kufanyia mawasiliano”.
Aidha kwa upande wa diwani wa kata hiyo Edward Haule amesema wanamshukuru mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kwa kuwapambania hadi wakapata mtandao wa TTCL sambamba na pongezi hizo amesema mtandao huo unachangamoto kwani baadhi ya maeneo haukamati kabisa huku unakokamata ukipiga unachelewa kuunganishwa.
Aidha kwa upande wa mbunge huyo amesema mawasilino ni jambo la msingi sana kwa jamii hivyo ataendelea kuwapambania ili kuhakikisha wanapata mawasiliano ya uhakika.
“Mawasiliano siyo kitu cha anasa ni jambo la msingi na lenye kuleta maendeleo maana ili biashara iende ni lazima ufanye mawasiliano mbalimbali ya kibiashara na vinginevyo”. Alisema Kamonga.