Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara, (MNRPC) Zacharia Mtigandi akifungua Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo na kuelezea mradi wa elimu ya afya ya uzazi Kwa wasichana na wanawake, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa MNRPC Mary Margwe na Katibu wa MNRPC Jaliwason Jasson
…………………………………………………………
Na Joseph Lyimo
Imeelezwa kuwa wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 17 wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, wameathirika na mimba za utotoni kwani kwa kipindi cha miezi 11 wasichana 183 wamepata ujauzito sawa na mimba 16 kila mwezi.
Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 mimba hizo za utotoni zilizoripotiwa 183, wasichana 21 wenye miaka 13 hadi 15 walipata mimba na wasichana 162 wenye miaka 16 hadi 17 walipata mimba.
Ofisa ustawi wa jamii wa wilaya ya Hanang’ Martha Sulle ameyasema hayo kwenye mkutano wa kutoa elimu juu ya haki ya afya ya uzazi uliondaliwa na klabu ya waandishi wa habari mkoani Manyara (MNRPC).
Mradi huo wa haki ya afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake kuanzia miaka 14 unatekelezwa na MNRPC kwa kushirikiana na shirika la Tanzania Women Fund Trust (WFT) wa miezi sita.
Sulle amesema ofisi ya ustawi wa jamii ya halmashauri hiyo ilipata taarifa za mimba kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo vituo vya afya, kwenye shule na dawati la polisi la jinsia.
Muuguzi msaidizi wa hosptali ya wilaya ya Hanang’ (Tumaini) Anasia Maliki akizungumza na walengwa wa mradi huo wa kata ya Endasaki amesema wasichana wana haki ya kuchagua watu wa kuwaoa na siyo kuchaguliwa na wazazi wao.
“Wasichana na wanawake wanatakiwa kutambua kuwa wanapaswa kuilinda miili yao wenyewe na siyo kila mtu aichezee kwani ni kitu cha thamani,” amesema Maliki.
Amesema wazazi na walezi wanatakiwa kuzungumza na wasichana wao kwani wakiwaacha bila kuwapa malezi bora wataendelea kubeba mimba zisizo tarajiwa wakiwa wadogo.
Hata hivyo, Katibu wa MNRPC, Jaliwason Jasson amewashukuru wasichana na wanawake wa kata ya Endasaki kukubali kupewa elimu ya haki ya afya ya uzazi kupitia mradi huo.
Jasson amesema mradi huo unaosimamiwa na MNRPC chini ya ufadhili wa Tanzania Women Trust Fund unatarajia kuwafikia wasichana na wanawake zaidi ya 120 wa kata ya Endasaki wilaya ya Hanang’ na kata za Riroda na Sigino za wilayani Babati.
Msichana wa kata ya Endasaki, ambaye ni mnufaika wa mradi huo, Magdalena Bayo amesema wasichana wengi wanakosa haki ya afya ya uzazi kutokana na elimu ndogo waliyonayo.
Bayo amewashukuru wanachama wa klabu ya waandishi wa habari wa mkoani huo na wafadhili wa mradi huo kwa kuwasogezea karibu elimu hiyo muhimu kwao.