Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameipongeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuratibu na kuendesha shughuli mbalimbali za mtangamano kwa manufaa ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mhe. Balozi Mbarouk ametoa pongezi hizo leo tarehe 23 Septemba 2021 jijini Arusha wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kati yake na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mhandisi Steven Mlote ikiwa ni ziara yake ya kwanza aliyoifanya kwenye Makao Makuu ya Jumuiya hiyo kwa lengo la kujitambulisha tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo.
Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Mbarouk alimweleza Mhandisi Mlote kwamba, amefarijika kutembelea Ofisi hizo na kujionea shughuli mbalimbali za uendeshaji zinazofanyika na kusisitiza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kuwa Jumuiya muhimu kwa nchi zote sita wanachama kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa katika kuziletea maendeleo endelevu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii nchi hizo.
Aidha alisisitiza kuwa, Tanzania itaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa michango yake ya mwaka ajili ya kuwezesha uendeshaji wa Jumuiya hiyo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mlote ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, alimshukuru Mhe. Mbarouk kwa kutenga muda na kutembelea Ofisi hizo na alitumia fursa hiyo kumweleza mfumo mzima wa uendeshaji wa Jumuiya kupitia Sekretarieti.
Mbali na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu, Mhe. Naibu Waziri pia alipata fursa ya kuzungumza na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Mhe. Ngoga Karoli Martin pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera ambapo kwenye mazungumzo yao viongozi hao walijadili masuala mbalimbali yanayohusu mchango wa Bunge na Mahakama hiyo kwenye Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kadhalika, wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Mbarouk alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Mkoa huo na Wizara hususan yale yanayohusu kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia sekta ya utalii ambayo imeshamiri kwenye mkoa huo.
Wakati huohuo, Mhe. Mbarouk amekitembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) ambacho ni moja ya Taasisi iliyo chini ya Wizara na kuitaka Menejimenti ya Kituo hicho kuendelea kuboresha utoaji huduma za kituo hicho lii kuendana ushindani uliopo kwenye sekta ya huduma ya utalii wa mikutano.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri aliwahimiza AICC kukamilisha mchakato wa kuanza ujenzi wa Kituo kipya cha Mikutano cha Kimataifa cha Mlima Kilimanjaro (MKICC) ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia mikutano mikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Vilevile alipata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na AICC ikiwemo Kumbi, Hospitali, Kiwanja kitakapojengwa kituo cha MKICC na nyumba za makazi zaidi ya 600 zilizopo maeneo ya Kijenge, Soweto na Barabara ya Range kwenye Jiji la Arusha.
Mhandisi Mlote akimkabidhi Mhe. Balozi Mbarouk zawadi ya machapisho mbalimbali kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki |
Mhe. Balozi Mborouk na Mhandisi Mlote wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe walioambatana nao wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kati yao |
Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Jaji Kayobera |
Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Mhe. Jaji Kayobera, Mhandisi Mlote (kulia) na Msajili wa Mahakama hiyo (kushoto) |
Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe.Ngoga Karoli Martin (kulia) mara baada ya kumaliza mazungumzo yao |
Mhe. Balozi Mbarouk akisikiliza maelezo kuhusu utendaji kazi wa Kituo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Kuratibu mwenendo wa magari ya mizigo hususan katika kipindi hiki cha ugonjwa wa UVIKO-19 |
Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mongella |
Kikao kikiendelea na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya AICC |
Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja naWajumbe wa Menejimenti ya AICC |