Taasisi ya Elimu Tanzania imekabidhi jumla ya vitabu 173,990 kwa ajili ya shule za Msingi na vitabu 2,714 kwa ajili ya shule za Sekondari, katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera, ambapo Mkuu wa wilaya ya Muleba Mh.Toba Nguvila amesema vitabu hivyo vitasaidia kuondoa upungufu wa vitabu kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya vitabu hivyo Mhe. Nguvila amewaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya, Ma Afisa Elimu pamoja na walimu wote kuhakikisha vitabu vinakwenda kutumika kama kusudio lilokusudiwa na Serikali la kwenda kuwafanya wanafunzi kuwa na vitabu vya kutosha ili kupata elimu bora.
“Tunataka wilaya ya Muleba iwe kinara wa elimu kwa maana ya ufaulu, kuongoza kitaifa na inawezekana kwasababu tayari Mhe. Rais ametupa vitabu kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania na nina amini vitabu hivi vinaenda kutumika kama vilivyokusudiwa,” ameeleza Mhe. Nguvila.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa shule za msingi, Mwalimu Severine Musyangi amesema kuwa vitabu hivyo vitasaidia kupunguza uhaba ulikuwepo wa vitabu kwa wanafunzi.
Amesema kwa sasa ujio wa vitabu hivyo utawezesha wanafunzi kupata kitabu kimoja kwa kila mwanafunzi mmoja.