Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la Mradi wa Maji Kifura wilayani Kibondo, Septemba 17, 2021. Kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na wa pili Kulia ni Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Tangi la Maji la Mradi wa Kifura wilayani Kibondo ambao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi, Septemba 17, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya maji, elimu na barabara.
Amesema lengo la utekelezaji wa miradi hiyo ni kuboresha maisha ya Watanzania, hivyo amewasihi wananchi wafanye kazi kwa bidii kila mmoja kwenye eneo lake na waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Septemba 17, 2021) wakati akiongea na wananchi wa wilaya za Kasulu na Kibondo mkoani Kigoma baada ya kuzindua ghala la kuhifadhia mazao katika kijiji cha Mvugwe na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji Kifura.
“Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kupeleka huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi wote nchini. Huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama kwa sababu anajua namna akinamama na vijana wanavyohangaika kutafuta maji.”
Naye, Meneja wa RUWASA mkoa wa Kigoma Mathius Mwenda alisema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 2.4 mkataba wake ulisainiwa Agosti mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Februari mwakani. Mradi huo utakapokamilika utakuwa na vituo 50 vya kuchotea maji.
Meneja huyo alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kunakwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Kifura, hivyo watahakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahiki.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa mradi wa ghala la kuhifadhia mazao, Mheshimiwa Majaliwa aliwapongeza kwa kubuni mradi huo na alisisitiza kuwa wananchi hao waendeleze ushirika wao na watumie ghala hilo kwa ajili ya kuuza mazao yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Joseph Rwiza alisema mradi huo uliogharimu shilingi milioni 464 unalenga kupunguza upotevu wa mazao, kutunza na kuongeza ubora wa mazao pamoja na kuwepo kwa soko la uhakika na bei yenye tija kwa wakulima.